Chongolo anapowamwagia upupu wapenda kupigiwa makofi na porojo

15Mar 2023
Augusta Njoji
SINGIDA
Nipashe
Chongolo anapowamwagia upupu wapenda kupigiwa makofi na porojo

CHAMA Cha Mapinduzi, kimetangaza kuangalia mienendo ya makada na viongozi wake, safari hii kikiwaonya kuwa hakitakubali wanaopenda kupigiwa makofi wakati wananchi wanateswa na kero mbalimbali.

Katibu Mkuu wa CCM, akiwa jukwaani mkoani Singida hivi karibuni. PICHA: AUGUSTA NJOJI

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo ameyasema hayo katika ziara ya siku sita mkoani Singida, akiambatana na sekretarieti ya chama hicho kuzungumza na wananchi kusikiliza kero na kuzitatua.

Anaongeza kuwa sifa ya kiongozi ni kuzungumzia matatizo na kuyatafutia ufumbuzi na kwamba CCM imepewa dhamana ya kuongoza nchi na viongozi hawaji kupiga porojo ila kusikiliza watu, kuchukua changamoto na kuzitatua na huko ndiko kuhangaikia mambo ya wananchi.

Katika ziara hiyo inayolenga kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025, anatembelea mashina ya CCM ili kuangalia uhai wa chama, ukaguzi wa miradi ya maji, vituo vya afya, hospitali na ujenzi wa miundombinu mkoani Singida.

MBOLEA YA RUZUKU

Akiwa Singida, Chongolo anapokea malalamiko ya mbolea ya ruzuku na kueleza kuwa CCM imetuma wachunguzi maeneo yaliyolalamikiwa  kwenye ugawaji wa pembejeo ikiwamo mbolea.

Anasema Rais Samia Suluhu Hassan aliamua kuwapunguzia mzigo wa gharama za pembejeo ambazo ni mbegu, mbolea na dawa za viuatilifu kwa kutoa ruzuku ya zaidi ya Shilingi bilioni 150.

Aidha, kwenye ziara hiyo anakishukia Kituo cha Uwekezaji (TIC) kwa kuishia kuwasajili wawekezaji kwenye makabrasha badala ya kuwatembelea kujua kero zao na kuzitatua ili uwekezaji uwe na tija kwa taifa.

Akikagua mradi wa kilimo cha alizeti unaotekelezwa na Kampuni ya Alfardaws, anasema kituo hicho kina jukumu la kutoa kibali kwa wawekezaji na kuhakikisha mahitaji muhimu yanamfikia kwenye eneo lake lakini hawafanyi hivyo.

“Bado tumeshindwa kutoka kuwa watu wenye kutimiza wajibu kuwa watu wenye kutafuta matokeo lazima kama nchi hili tulifanye kwa dhati ya mioyo yetu, hatuwezi kuwa na namba ya wawekezaji tuliowasajili hatujui huko wanafanya nini, wanawezeshwaje kufikia uwekezaji uliokusudiwa,”anasema.

Katibu huyo anasema mwekezaji Alfardaws kwa zaidi ya miezi minne ana tatizo la kutounganishiwa umeme ambao upo kilometa tatu na kutaka viongozi kutimiza wajibu.

Akiwa mgodi wa dhahabu Shanta, anasema kumekuwa na tatizo la umeme kwa wawekezaji na kuitaka Tanesco kuweka msukumu wa kujenga vituo vya kupoozea umeme kwenye maeneo yenye uwekezaji mkubwa ikiwamo ukanda wa Singida.

UKATILI KIJINSIA

Chongolo anaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kuweka mfumo wa kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa jamii baada ya wananchi wa maeneo ya Singida kulalamikia kukithiri kwa vitendo hivyo.

“Hatuwezi kuwa na nchi ambayo inaacha matendo ya ukiukwaji wa haki za binadamu na sisi tukasema tupo na amani ni lazima matendo haya yashughulikiwe hata kama ni machache.”

Anatoa maelekezo kwa Wizara ya Afya ibainishe mpango wa Bohari ya Dawa (MSD) wa kupeleka dawa na vifaa tiba kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati zilizojengwa  ili kuhudumia wananchi.

 

"Nakwenda kukaa na Waziri wa Afya aniambie mpango wa MSD kupeleka dawa na vifaa tiba kwenye hospitali na vituo vya afya vilivyojengwa n, majengo yakikamilika yanapaswa kutoa huduma,"anakumbusha.

 

Katika hatua nyingine,anamtaka Mwenyekiti wa Halmashauri ya Singida, Elia Diga kutoa majibu kwa wananchi kuhusu kulazimishaa kulipa fedha za matibabu kabla ya kupata huduma.

 

Akiwa katika Kijiji cha Mntiko, anapokea malalamiko hayo ambayo mkazi wa kijiji cha Mtinko, Jamal Kyoka, anasema wanapokwenda hospitali mtu anatakiwa kutibiwa ndipo alipe fedha lakini kwasasa mgonjwa  asiye na fedha anakuwa hatarini.

Anasema anaweza kufia kwenye benchi kwa kuwa hatapewa huduma bila kutoa fedha kwanza, ndipo

Katibu Mkuu Chongolo anaposema wananchi wapate huduma kisha walipe, akimtaka mwenyekiti huyo kuondoa malalamiko hayo kwa wananchi.

 

KWA SERIKALI

 

Akihitimisha ziara anatoa maelekezo manne kwa serikali baada ya kubaini kero mbalimbali zinazowakabili wananchi kwenye sekta ya afya, elimu na kilimo.

Anaelekeza hospitali zinazojengwa wilayani na zilizokamilika zianze kutoa huduma kwa wananchi ili kuzuia vifo vya mama na watoto.

Anasema CCM inaelekeza serikali na kuweka msukumo wa kuhakikisha wahudumu wa afya wanaletwa kwa idadi ya kutosha ili huduma zitolewe kwenye hospitali hizo ili kuleta matokeo halisi yaliyokusudiwa ya kusogeza huduma kwa wananchi.

Pia anasema kuna baadhi ya maeneo fedha kutoka serikali zimechelewa kumalizia majengo ya zahanati yaliyojengwa na fedha za wananchi ikiwamo Kijiji cha Ngimu, Kinambeu na kutaka serikali ipeleke fedha haraka ili kukamilisha. ujenzi.

Kuhusu sekta ya elimu, anaelekeza kujenga shule za kidato ya tano na sita ndani ya miezi mitatu ili kupanua wigo wa kupokea wanafunzi kutoka asilimia 25 hadi 70.

Akizungumzia kuhusu kilimo, anasema mkoa huo unalima kwa kiwango kikubwa alizeti ili kupunguza utegemezi wa mafuta ya kula kutoka nje hivyo wajibu wa serikali ni kulinda bei ya mafuta na wakulima wa alizeti kwa kuzuia uingizaji wa mafuta bila kufuata taratibu.

Anawahakikishia kuisukuma serikali na kuwajibika kupeleka pembejeo za mbolea ya ruzuku kwenye maeneo yaliyokaribu na wakulima katika vifungashio tofauti vidogo tofauti na sasa mbolea ipo mifuko ya kilo 50.

“Tunaelekeza serikali kuanzia msimu ujao ilete mbolea kwenye vifungashio tofauti kilo 10, 25 na 50 ili mwananchi yeyote anunue kwa kiwango chenye uhitaji na si vinginevyo” anasema.