BOLA AHMED TINUBU

15Mar 2023
Gaudensia Mngumi
NIGERIA
Nipashe
BOLA AHMED TINUBU
  • Ndiye rais ajaye Nigeria, kuapa Mei 29, ni bepari ila chanzo utajiri hakijulikani *Ana msururu wa kashfa,kuuza ‘unga’, ufisadi na kesi Marekani

NI mfanyabiashara maarufu akimiliki kuanzia vyombo vya habari, usafiri wa anga hadi majengo ya kila aina, ndiye Bola Tinubu, rais mteule wa Nigeria.

Kwa sasa anajiandaa kula kiapo asubuhi ya Jumatatu Mei 29, katika Uwanja wa Eagle huko Abuja jiji kuu la Nigeria, kuwa rais wa taifa hilo.

Akiwa na miaka 70, yeye na mgombea mwenza Seneta Kashim Shettima wa jimbo la Daura, wameshinda urais wa taifa hilo lenye watu wengi zaidi barani Afrika kwa kura milioni 8.8, kwa mujibu wa matokeo ya mwisho ya uchaguzi, yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Nigeria (INEC).

Bola Tinubu, au ‘political godfather’ "mungu wa kisiasa" anasifika kwa umahiri wake,mikakati na ushujaa kwenye siasa, na kushinda kinyang'anyiro kikali cha kumrithi Muhammadu Buhari kama rais wa Nigeria.

Ni nchi yenye watu zaidi ya milioni 120, lakini rais akishinda kwa kura milioni 8.8.

Tinubu anaelezwa kuwa hakuwahi kuficha azma yake ya kutaka kuwa rais wa Nigeria kwani bilionea huyo ambaye wengi humwita ‘kikongwe’ na kizee cha miaka 70 ametimiza lengo lake la maisha kwa kushinda urais wa taifa hilo japo kwa kura kiduchu milioni 8.8.

Licha ya maswali mengi kuhusu afya yake na madai ya ufisadi, kuuza dawa za kulevya, yaliyopita, gavana huyo wa mara mbili wa Lagos atamrithi Muhammadu Buhari, jenerali wa zamani wa jeshi, ambaye Tinubu anajisifu kuwa ndiye aliyesaidia kumuweka madarakani.

Tinubu anaangalia mbele, akiamini kuwa ushindi ni ushindi hata kwa goli la mkono, licha ya chama chake tawala cha All Progressives Congress (APC) kinakabiliwa na shutuma za udanganyifu katika uchaguzi uliofanyika Jumamosi Februari 25, 2023 kutoka kwa wapinzani wake wawili wakuu. Lakini maofisa wa uchaguzi na APC wametupilia mbali madai hayo.

 

HAKUBALIKI NYUMBANI

Mara nyingi Tinubu hujulikana kama chifu wa "Jagaban", Kwa Kiyoruba ambalo ni kabila kubwa la Nigeria, Jagaban ni jina au cheo anachopewa shujaa na jasiri, aidha ni mnyama asiyeogopa chochote!

Tinubu ametumia miaka mingi kujenga ngome yake kisiasa Lagos na kuunda mtandao wa kitaifa wa mawasiliano kutoka kwa vyama vya ushirika vya wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo na pia jumuiya za wasafirishaji hadi mashirika na taasisi za kisiasa akisaka kuungwa mkono.

Hata hivyo, ngome ya Lagos na wapambe aliodhani anao , katika matokeo yaliyoleta mshangao mgombea walimtosa. Mpinzani wake wa Chama cha Labour, Peter Obi, alimgaragaza kwenye jimbo la Lagos alilodhani ni ngome yake ya jadi.

"Unashinda baadhi ya maeneo,lakini unapoteza kwingine ," Tinubu anasema kuhusu matokeo hayo, akiwataka wafuasi wake kuwa watulivu na kujiandaa kwa ushirikiano.

Siku kadhaa baadaye, kiongozi huyo alifanya kampeni kwa kauli mbiu "Ni zamu yangu", alithibitishwa kuwa mshindi wa urais, licha ya kupata kura kiduchu, ambazo wagombea wawili Peter Obi wa Labour na Abubakar Atiku wa chama PDP walimzidi kwa mbali.

 

ANAANZIA MAREKANI

Tinubu aliyezaliwa miaka 70 iliyopita katika eneo la kusini-magharibi la Nigeria ni Myoruba, aliyesoma uhasibu nchini Marekani na alifanya kazi kwenye kampuni kadhaa za Amerika, ikiwa ni pamoja na mtunza hazina katika kampuni kubwa ya mafuta ya ExxonMobi.

Anaanza kuwa mwanaharakati wa kisiasa kabla ya kuwa seneta na baadaye gavana wa Jimbo la Lagos, ambalo analiongoza kutoka 1999 hadi 2007.

Wafuasi wa Tinubu wanaamini mafanikio ya Lagos yanayonekana leo ni kazi yake, wakitamba kuwa jimbo la jiji kubwa lenye uchumi bora zaidi nchini Nigeria haliwezi kusahau mchango wa Rais Mteule.

Hata hivyo, wakosoaji wengine wanasema hizo ni porojo za wafuasi waliochoka wa Tinubu, wakiamini kuwa mafanikio hayo ni kazi za siasa za ustawi wa Gavana Lateef Jakande, aliyeongoza jimbo hilo kuanzia 1979 hadi 1983, ambaye aliweka misingi ya Lagos ya leo.Jiji hilo lina watu milioni 21.

Akielezewa na washirika wake kama mwanamkakati mahiri wa kisiasa, alianzisha na kufadhili masuala ya kidemokrasia ambayo baadaye yalifanikisha kuundwa Action Congress of Nigeria, na kisha kufikia chama cha APC.

Anaelezwa kuwa na mchango mkubwa katika kuleta pamoja vikundi vya APC, na kumsukuma Buhari kushinda mwaka wa 2015 na kusaidia ushindi wa kumaliza miaka 16 madarakani kwa mpinzani wa People's Democratic Party (PDP).

Uchaguzi wa Buhari, ushindi wa kwanza wa upinzani nchini humo, pamoja na kuchaguliwa tena kwa 2019, ulichangiwa kwa sehemu kubwa na ushawishi wa kisiasa wa Tinubu, ambaye huenda amelipa fadhili kwa kumpigia debe kuwa mgombea na kisha kuwa rais mteule mwaka huu.

 

TUHUMA ZA UFISADI

Malumbano yanayomzunguka Tinubu wakati huu ni kuhusu shughuli zake za kifedha wakati akiwa madarakani kwenye jimbo la Lagos.

Anaaminika kuwa mmoja wa wanasiasa matajiri zaidi wa Nigeria na baada ya kuondoka madarakani anashutumiwa kwa ufisadi, utakatishaji fedha na kuendesha zaidi ya akaunti 12 za benki za kigeni.

Hata hivyo, hakuwahi kushtakiwa wala kuhojiwa na muda wote amekuwa akikanusha makosa wala tuhuma hizo.

 

‘MZUNGU WA UNGA’

Katika kampeni, wakosoaji wa PDP walimtaja kama "mchafuko’, mwoga na aliyeathiriwa na  unga akijihusisha na dawa za kulevya", wakimaanisha wana wasiwasi na afya yake na pia wanazungumzia kesi ya mwaka 1993 katika mahakama ya Marekani ambayo ilitaifisha mali zake zinazohusiana na dawa za kulevya kutoka kwenye akaunti yake ya benki za Marekani

Chanzo cha utajiri wake hakijajulikana lakini ana maslahi katika ubia kadhaa wa kibiashara, kutoka vyombo vya habari na usafiri wa anga hadi ushauri wa kodi, hoteli na umiliki wa mali isiyohamishika ya ardhi na majengo.

Mkosoaji wake anamtaja kama "mwanasiasa mchoyo" ambaye amekusanya vyanzo vikuu vya mapato kutoka Lagos na kujitengenezea utajiri mkubwa akiwaacha hoi maskini.

CHANZO: Al JAZEERA