Kwanini? Ni kupitia malezi ya mtoto wake, kwani baada ya mtoto bintiye kupata ujauzito akiwa mwanafunzi, badala ya kuwa mkali na kuchukua hatua kulingana na mazoea na utamaduni uliotawala visiwani.
Zanzibar kumezoeleka kwamba mtoto akiwa chini ya uangalizi wa walezi au wazazi na akapata ujauzito, hupata kipigo, kufukuzwa au kutengwa na familia.
Ni tabia iliyoeleka hata nje ya visiwa hivyo. Kuna wazazi wanaofikia hatua ya kuchukua sheria mkononi, huku baadhi ya watoto nao kwa hofu huchukua maamuzi magumu, ikiwamo ama kujiua au kutoa mimba.
Hali ni tofauti kwa mzazi Waziri Muhammed, ambaye bintiye alipata ujauzito akiwa na umri wa miaka 16.
Yeye alichukua staili ya kuzidisha upendo kwa binti yake na kuamua kumuendeleza kielimu baada ya kujifungua na sasa kuna mafaniko makubwa.
Anaeleza kuwa binti yake alipata ujauzito akiwa anasoma kidato cha pili mwaka 2013 na kuamua aendelee na masomo.
Binti baada ya kurudi shule alifanya vizuri kwa kufaulu kidato cha pili na akajiunga na kidato cha tatu. Baadaye alifanya vyema baada ya kidato cha nne na kuendelea na kidato cha tano.
Akizungumza nyumbani kwake, anasema baada ya binti kupata ujauzito, aliamua kumuendeleza kielimu, akiamini elimu ndio itakayomsaidia katika maisha ya baadaye.
“Baada ya kugundua mtoto wangu ana ujauzito, niliripoti Polisi, lakini nilivunjika moyo baada ya Polisi kunitaka nikamtafute aliyempa ujauzito mtoto wangu nimpeleke kituo cha Polisi, wakati mhalifu huyo ameshakimbia nchini,” anasema.
Anasema ni tukio lililomvunja moyo kuendelea na kesi hiyo na ndipo alipokwenda kufuata ushauri kwa Mkuu wa Shule aliyokuwa akisoma binti yake, kama kuna uwezekano wa kuendelea na masomo akiwa na ujauzito.
Anasema mwalimu huyo alimueleza upo uwezekano wa binti kuendelea na masomo kulingana na sheria ya elimu.
Mzee Muhammed anasema baada ya kufuata utaratibu na kupewa maelekezo, alimhoji binti kama yupo tayari kuendelea na masomo na alikubali.
Anasema kitendo cha binti yake kukubali kuendelea na masomo, kilimpa faraja kubwa na aliongeza upendo zaidi kuhakikisha anafika mbali kielimu.
“Nashkuru binti yangu alinisikiliza, aliendelea na masomo na sasa amefaulu kidato cha nne kuelekea kidato cha sita,” anasema Muhammed.
Kwa mujibu wa mzee huyo, binti yake ameshajifungua mtoto wa kike na yeye akajiweka tayari kwa malezi ya binti na mjukuu, bila ya kuhitaji msaada kwingineko.
Ushauri wake kwa wazazi wenzake kwa watoto wao wanaopata mimba shuleni, kwamba wasichukue hasira, wawaendeleze na masomo.
“Baada ya mtoto wangu kupata ujauzito nilikuwa nipo karibu naye sana na huwa namshauri kuendelea na masomo,” anasema.
BINTI ANENA
Asia Waziri Muhammed (19), akiwa na mtoto wake mwenye umri wa miaka miwili na miezi mitano, anasema hakutarajia kupata mimba akiwa na umri mdogo, lakini ilimtokea baada ya kubakwa na mtu ambaye hakuwa na uhusiano naye kimapenzi.
Anasema tukio lililomtokea mwaka 2012 akiwa njiani kwenda dukani, saa 1.00 usiku na ilikuwa mara ya kwanza kuonana naye.
Anaendeleza simulizi kwamba baada ya ubakaji, mwanaume huyo alimtaka aondoke na alirejea nyumbani akiwa na hofu ya kuchelewa, huku akishindwa kueleza chochote hadi alipokuwa na mimba ya miezi minne.
Sababu ya kuficha kilichomtokea, ni hofu aliyotishiwa na mbakaji, aliyemtaka asieleze kwa mtu.
Asia anasema akiwa anaendelea na masomo, ndipo aligundua ana mimba, kutokana maumbile yake kubadilika.
Anasema baadhi ya wana jamii walianza kumnyanaypaa kutokana na hali hiyo, ingawa anakiri wazazi wake walikuwa naye bega kwa bega, aliyempa mimba alimkana na kisha akakimbia.
“Nawashukuru wazazi wangu na walimu wangu wa shule, pamoja na baadhi ya wanafunzi wezangu.
“Hawakunitenga wala kuninyanyapaa kutokana na ujauzito niliyokuwa nao. Walikuwa wakinipa moyo niendelee na elimu,” anasema.
Ananukuu baadhi kauli za unyanyapaa dhidi yake kwamba:”Unasoma nini badala ya kulea tumbo lako! Kama ungekuwa unataka kusoma ungebeba ujauzito?”
Asia ansema hilo halikumvunja moyo alizidisha bidii na kufanikiwa kufaulu kidato cha pili. Alihudhuria masomo hadi siku chache kabla ya kujifungua na alipumzika wiki mbili tu baada ya kujifungua na akarejea darasani.
Anasema utaratibu wake wa kuhudhuria masomo, alikuwa anamuacha mtoto kwa bibi yake na aliporudi ndiyo alimnyonyesha mwanawe.
Asia anasema aliendelea na masomo kwa mfumo huo na ameufanikiwa kufaulu mtihani wa kidato cha nne, sasa yuko katika orodha ya waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu.
“Matokeo yametoka hivi karibuni baada ya kupata taarifa kuwa nimefaulu, nimefurahi sana na nina imani kuwa ndoto zangu zitafanikiwa. Maana malengo yangu baada ya kumaliza masomo nataka kuwa mwandishi wa habari,” anasema Asia.
Anaeleza kinachomvuta kuwa mwanahabari ni kwamba apate fursa ya kuwa mwelimishaji wa jamii na hasa masuala ya wanawake na watoto.
Anawatetea wasichana wanaoopata ujauzito kwamba si wote wanautaka. Anaongeza:”Nilipopata ujauzito, baadhi ya wanajamii walikuwa na fikra potofu kuwa hali niliyokuwa nayo nimefanya kwa makusudi”.
MWALIMU WAKE
Mkuu wa Shule ya Dunga anakosoma Asia, Mwalimu Fadhil Hassan Haji, anasema Asia alianza darasa la kwanza hadi kidato cha nne shuleni hapo. Anasifu bidii yake, hata alipopata ujauzito.
Anasema mbali na upole na uhodari wake, hata baada ya kupata mimba aliendelea vyema na masomo akiwazidi wanafunzi wenzake.
“Siyo wanafunzi wengi wanaopata ujauzito wakataka kuendelea na masomo. Wengi hutaka kuolewa au kulea mtoto wake,” anasema.
Anaongeza kuwa Sheria ya Elimu Zanzibar iliyofanyiwa marekebisho mwaka 1993, inatoa fursa kwa mwanafunzi atakayepata ujauzito, haki ya kuendelea na masomo.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa shule, kabla ya marekebisho mwanafunzi anayepata ujauzito anafukuzwa shule.
Mrajiso wa Elimu Zanzibar, Siajabu Suleiman Pandu, anasema sheria hiyo haitoi fursa kwa mwanafunzi aliyeolewa kuendelea na masomo.










