‘Mahausigeli’ walivyoingizwa kwenye semina inayowanoa

25Apr 2023
Sabato Kasika
DAR ES SALAAM
Nipashe
‘Mahausigeli’ walivyoingizwa kwenye semina inayowanoa
  • kwenda sawa na yanayowakuta

KUNA baadhi ya wafanyakazi majumbani wanakiri kupitia unyanyasaji wa aina mbalimbali, ikiwamo mashambulio ya aibu, ngono na mateso mengineyo ya hatari kwa afya zao, kwani seketa hiyo imetawaliwa na mabinti wenye umri chini ya miaka 18 katika umaarufu wao ‘wadada wa kazi’ au ’wasichana wa kazi.’

‘Wadada wa kazi’ wakiwa mafunzoni katika Chuo cha Ustawi wa Jamii, Dar es Salaam. PICHA: SABATO KASIKA.

Hata hivyo, inaelezwa taarifa nyingi za idadi yao majumbani katika kaya, hazipatikani kirahisi kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo waajiri kutokuwa tayari kuweka wazi. Ni haki inayoifanya Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Dar es Salaam, kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa malezi na makuzi wafanyakazi hao mkoani Dar es Salaam, ili wajitambue haki zao, kuepuka mazingira yanayowagusa. 

Mkuu wa taasisi hiyo, Dk. Joyce Nyoni anasema miaka ya karibuni kumekuwapo kelele nyingi za malalamiko kuhusu malezi na tabia za watoto, hivyo wanaamua kutoa mafunzo kwa wasaidizi hao 100 wa majumbani. 

"Kinamama wengi wanaondoka asubuhi na kurudi jioni, watoto wao wanakaa na ‘madada wa kazi’, lakini bahati mbaya hawana uelewa kuhusu malezi na makuzi ingawa wana mchango mkubwa katika kulea," anasema Dk. Joyce. 

Pia, anafafanua ni mchakato ambao ‘madada wa kazi’ nao kuna siku watakuwa mama, hivyo ni muhimu wakaelewa wanavyopaswa kulea mtoto, kulingana na mabadiliko yaliyoko. 

WALIVYONOLEWA DARASANI

 

Dk. Joyce anafafanua walichokifanya, ni kuwajengea uwezo watambue na kuepuka unyanyasaji unaoweza kuwakumba, ukiwamo wa kingono ambao ni hatari kwa afya zao. 

Anasema uelewa unamsaidia mtu kujitambua, pia kutambua hatari, hata akaepuka, akimini mafunzo hayo ya watumishi, yatawafanya kuwa mabalozi azuri waliko majumbani. 

"Tumewafundishwa kumuelewa mtoto na kuwa na msaada chanya katika maendeleo na makuzi ya mtoto, kwa kuwa na wao kama binadamu wana mapungufu yao," anadems, akianisha ukuaji mtoto uko kimwili, kiakili, kiroho na kijamii, hivyo wakiona tatizo wanapaswa kutoa taarifa kwa wazazi au walezi wa mtoto. 

Anafafanua kwamba, wakati ukatili unatokea, ‘wadada’ hawawaelewi watoto na kwamba wakimuelewa, watajua namna ya kuwasaidia, mabosi nao wawafanye wawe katika mazingira ya kujiamini anapolea mtoto. 

“Ni mafunzo yaliyoambatana elimu ya jinsi ya kukabiliana na misongo ya mawazo, matumizi sahihi ya fedha na kuweka akiba, usafi pamoja na mawasiliano kwa mabosi wao. Ni namna inahuisha hisia ya kutoweza kukabiliana na mahitaji yanayotokana na kazi, mahusiano, shinikizo za kifedha na hali nyingine za maisha. Sisi sote tunapitia msongo wa mawazo kwa njia tofauti," anasema. 

Anafafanua kwamba, mara nyingi mtu anaweza kushindwa kujua kuwa anachopitia ni msongo wa mawazo na kwamba, akiwa anapata mabadiliko hayo, kuna uwezekano kuwa anakabiliwa na msongo wa mawazo. 

Kwa mujibu wa Dk. Nyoni, msongo wa mawazo unaweza kumsababisha mtu akapoteza hamu na tamaa ya kufanya alichokuwa akifurahia awali, akihisi kufa moyo au kukosa tumaini akitawaliwa na hisia mbaya, binafsi akitafsiri ‘amefeli’ maisha. 

"Tumeona ni muhimu tuwape elimu watambue hayo, kutokana na ukweli kwamba wanapitia changamoto nyingi ambazo wakati mwingine husababisha wafanye ukatili kwa watoto wa mabosi wao," anasema. 

Mhadhiri wa taasisi hiyo na Mratibu wa Kitengo Ushiriki Jamii, Dunstan Haule aliyeshitriki kufundisha mafunzo hayo, anasema yatawasaidia katika usafi, kujilinda na namna ya kuwasiliana pale wanapokuwa na changamoto ndani ya familia.

"Pia, upande wa akiba, ninaamini mafunzo waliopata yatawasaidia kutambua umuhimu wa kujiwekea akiba benki, kwa ajili ya maisha yao ya baadaye na sio kutumia fedha yote ya mshahara," anasema Haule. 

WANUFAIKA WANENA 

Lucy Lazer, ni mnufaika wa mafunzo hayo, anayeeleza amejifunza

namna ya kuepuka unyanyasaji kingono, kukaa na watoto na kucheza nao, hata kutambua mabadiliko katika makuzi yao. 

"Nitakwenda kutumia mafunzo haya kwa vitendo, ili kufanya kazi yangu kwa ufanisi zaidi kule ninakoishi, kwani nimejifunza mengi, hasa namna ambavyo nitaweza kuepuka unyanyasaji kukaa na watoto," anasema Lucy. 

Mnufaika mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Martha Kavindi, anaeleza imani yake kwamba, mafunzo yatamjengea uwezo wa kulea watoto wa mabosi wao vizuri na hata wao wenyewe kujiandaa kuwa mama wa baadaye. 

"Ni wazi kwamba kila mmoja wetu amejua hatua za ukuaji wa mtoto kimwili, kiakili, kiroho na ukuaji wa kijamii na amejua watoto anaowalea wanapitia hatua zote kama tulivyofundishwa," anasema Martha. 

Mshiriki ambaye ni mfanyakazi wa ndani na hakupenda jina lake kuandikwa gazetini, anakiri wanapitia changamoto nyingi, ikiwamo wazazi wa watoto kutotoa nafasi ya kuwasikiliza, hali anayodai inayowachosha. 

“Tunashindwa kueleza changamoto walizonazo watoto wao katika makuzi, yaani wazazi wana majukumu mengi wanakosa nafasi ya kuwasiliana nasi," anasema.

 

 

 

Top of Form

Bottom of Form

 

Top of Form

Bottom of Form