Tembo aua mzee wa miaka 74

19Jun 2022
Thobias Mwanakatwe
Ikungi
Nipashe Jumapili
Tembo aua mzee wa miaka 74

​​​​​​​MZEE mwenye umri wa miaka 74, Nyeusi Maghiya, mkazi wa Kitongoji cha Kakamega, Kijiji cha Mlumbi, Kata ya Mang'onyi wilayani Ikungi mkoani Singida, ameuawa kwa kukanyangwa na tembo wakati akivuna mtama shambani.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro, ambaye alifika katika kijiji hicho haraka baada ya kupewa taarifa, alisema tukio hilo limetokea jana majira ya saa tatu asubuhi baada ya tembo watatu kuvamia katika kitongoji hicho na kisha kumkanyaga mzee huyo na kumvunja miguu,mikono na mbavu na kusababisha umauti.

Tukio hilo ni la pili kutokea katika kata hiyo mwaka huu ambapo wiki tatu zilizopita, tembo alimuua mtoto mwenye umri wa miaka mitatu katika Kijiji cha Ituntu.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mlumbi, Issa Abdalla, na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kakamega, walimweleza Mkuu wa Wilaya kuwa tembo wamekuwa wakipita mara kadhaa katika kijiji vya Kata ya Mang'onyi na kusababisha vifo na uharibifu mkubwa wa mazao shambani.

Walisema kutokana na hali hiyo, wananchi wamekuwa na hofu na wanafunzi kuogopa hata kwenda shuleni kwa hofu ya kushambuliwa na tembo ambao wameendelea kuwa tishio katika kata hiyo.

Wenyeviti hao waliiomba serikali kufanya haraka utaratibu wa kuwaondoa tembo hao ili wananchi wawe na amani na kuendelea na shughuli zao za uzalisha hususani katika kipindi hiki ambacho ni cha mavuno mashambani.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Muro, akizungumza na wananchi katika eneo la tukio, alisema serikali imeandaa programu ya kuyatambua maeneo ambayo yamekuwa sugu kwa mwingiliano wa wanyama kupita ili kuhakikisha wanaondolewa, ili wasiendelee kuleta madhara zaidi.

"Wilaya yetu imekumbwa sana na changamoto hii ya tembo na tumeshatoa taarifa kwa wenzetu wa maliasili ambapo wiki tatu zilizopita tembo aliua mtoto wa miaka mitatu na leo (jana) tumepata msiba wa mzee wetu kuuawa na tembo, tumeshatoa taarifa waondolewe," alisema.

Muro aliwaomba wananchi wakiona tembo, wasianze kuwakimbiza na kuwashambulia kwani wamekuwa wakipita tu na tembo anapoona anashambuliwa, anajihami na kuanza kushambulia.

"Ombi langu kwenu wakati serikali inaendelea kupambana na changamoto hii, wananchi mchukue tahadhari ya maisha yenu. Unapoona tembo, rudi nyumbani, chukua watoto wako mnajifungia ndani na mtatoka nje mtakapoelezwa na viongozi wenu wa kijiji au kitongoji kama tembo wameshaondoka," alielekeza.

Alisema wananchi wasijaribu kuwashambulia au kuwakimbiza kwa kuwa hawana utalaamu na wanyama hao kwa kuwa kipindi hiki cha mavuno, kimekuwa na idadi kubwa ya wanyama kama tembo kupita.

Muro pia aliwataka wananchi wawe wanatunza vyakula ndani ya nyumbani kwani wanyama wanaposikia harufu ya chakula, hufika kwenye makazi ya watu kutafuta chakula.

Kata za Mang'onyi na Ntuntu tembo wamekuwa wakipita mara kwa mara na katika historia inaonyesha maeneo hayo ni ushoroba ambao walikuwa wakipita miaka ya zamani kabla watu hawajaongezeka na kuweka makazi kwenye maeneo hayo ya ushoroba wa tembo.