Khamis Hamza Khamis alitoa rai hiyo jana alipofanya ziara ya kikazi ya kujionea uzingatiaji wa sheria ya mazingira katika kiwanda cha kuzalisha mafuta ya alizeti cha Pyxus kilichoko eneo la Kizota jijini Dodoma.
Alisema mataifa mbalimbali yaliyoendelea hutoa fedha kwa nchi zinazoendelea kwa kutambua kuwa wao ndiyo chanzo cha uharibifu wa mazingira kutokana na hewa ya ukaa wanayozalisha.
Naibu waziri huyo alisema viwanda havina budi kuchangia shughuli za mazingira na za kijamii kwa ujumla zikiwamo upandaji miti, utoaji elimu kuhusu uhifadhi na utunzaji wa mazingira.
"Ninawapongeza kiwanda hiki cha Pyxus nimesikia mnafanya shughuli za kupanda miti katika eneo lenu, hivyo ninatoa wito kwa viwanda vingine nchini viwe na utaratibu huu ili tuhakikishe tunatunza mazingira," aliagiza.
Aliwataka wamiliki wa viwanda vyote nchini wawe na mfumo mzuri wa kutibu na kudhibiti majitaka ili kuhakikisha hayatiririki na kumwagika kwenye makazi ya watu, hali inayoweza kuhatarisha afya na mazingira.
Pia alielekeza viwanda vidhibiti moshi unaotokana na shughuli za viwandani usisambae katika makazi ya watu, hali inayoweza kuwasababishia matatizo ya kiafya. Vilevile, alielekeza viwanda vidhibiti kelele zinazotokana na mashine za viwandani zisiwe kero kwa wananchi kwa kuwa zinaweza kuwasababishia matatizo ya masikio.
Meneja Rasilimaliwatu wa Kiwanda cha Pyxus, Gideon Mutta, alisema uongozi wa kiwanda hicho umepokea maelekezo hayo na kuahidi yatashughulikiwa.
Hata hivyo, meneja huyo alisema wanakabiliwa na shida ya miundombinu ya mfumo wa majitaka, akiiomba Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA) kuwasaidia na kuona namna ya kuwaunganisha na mfumo wa Jiji la Dodoma.










