ACT: Wananchi walipwe fidia kabla ya ubomoaji

19Jun 2022
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
ACT: Wananchi walipwe fidia kabla ya ubomoaji

​​​​​​​CHAMA cha ACT Wazalendo kimeitaka serikali kusitisha mpango wa kuvunja Soko la Manzese B lililoko Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma hadi wafanyabiashara wa soko hilo wataposhirikishwa vya kutosha na kulipwa fidia.

Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu.

Rai hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, alipokwenda sokoni huko na kufanya kikao na wafanyabiashara wa soko hilo.

"Nimeambiwa serikali inataka kuvunja soko hili na kujenga soko jipya la kisasa. Hatua hiyo ni njema, lakini ninafahamu soko hili lilijengwa na ninyi wafanyabiashara na mkataba wenu na halmashauri unamalizika mwaka 2025.

"Hivyo basi, si haki kwa serikali kutaka kulivunja kabla ya kuzungumza na ninyi na kuwalipa fidia. Nimeelezwa kuwa mmepewa notisi ya kuhama ifikapo tarehe Mosi Julai, 2022.

"Ninamuomba Waziri Mwenye dhamana ya TAMISEMI, Ndugu Innocent Bashungwa kuingilia suala hili. Mradi huu hauwezi kutekelezwa kabla ya kuwalipa fidia wafanyabiashara na kuwatafutia maeneo mazuri ya kwenda.

"Pia, mradi ukikamilika, wafanyabiashara wa sasa wapewe kipaumbele kupewa maeneo," Katibu Mkuu huyo alifafanua.

Alitoa rai kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwamulika wawakilishi wake wa ngazi za chini kwa kuwa baadhi ya uamuzi wao unawaumiza wananchi maskini na hivyo kuipaka matope serikali.

"Soko hili lina wafanyabiashara 700. Unapowaumiza watu 700, unakuwa umeumiza maelfu ya familia zao na kuwajengea chuki na serikali," alionya.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo wa ACT Wazalendo amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kuhakikisha serikali za vijiji zinazingatia taratibu za uuzaji wa ardhi ya kijiji.

Alitoa rai hiyo juzi alipotembelea Kijiji cha Kipingo kilichoko Jimbo la Madaba, wananchi wa kijiji hicho wakilalamika kuhusu kitendo cha Serikali ya Kijiji kuuza zaidi ya ekari 1,500 za kijiji bila baraka za Mkutano Mkuu wa Kijiji.

Wanakijiji hao walidai kuwa wale ambao wamekuwa wakihoji dhidi ya suala hilo, wanakamatwa na Jeshi la Polisi, kupigwa na kubambikwa kesi.

Aliwaahidi wanakijiji hao kuwa ACT Wazalendo kupitia Kamati ya Kuisimamia Serikali ya Wasemaji wa Kisekta, italifuatilia suala hilo.