Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa habari nchini humo, Mohammed Idris, ambapo amesema, ndugu wa wanafunzi hao wanasema watekaji nyara wameomba fidia kubwa ili kuwaachilia wanafunzi waliotekwa nyara shuleni mwao Alhamisi iliyopita katika kijiji cha Kuriga kaskazini magharibi mwa Jimbo la Kaduna.
Magenge ya wahalifu mara nyingi huteka nyara watu wengi kaskazini mwa Nigeria, yakilenga shule, vijiji na barabara kuu.
Katika miaka mitatu iliyopita, mamia ya wanafunzi walitekwa nyara. Waathirika wa utekaji nyara nchini Nigeria mara nyingi huachiwa huru baada ya mazungumzo na mamlaka, ingawa maafisa wanakanusha malipo ya fidia kufanyika.
Kwa kuzingatia msimamo rasmi wa serikali, Waziri Idris amesema Rais Tinubu amewaambia maafisa wa usalama wanaowatafuta wanafunzi kuhakikisha “hakuna hata senti moja inayolipwa”.
“Rais ameviagiza vyombo vya usalama kwamba kwa sababu ni suala la dharura lazima vihakikishe watoto hawa na wale wote waliotekwa nyara wanarejeshwa nyumbani wakiwa salama,” amewambia waandishi wa habari kufuatia mkutano wa baraza la mawaziri katika mji mkuu Abuja.