Mwalimu Mkuu adaiwa kumlawiti mwanafunzi na kisha kumpa sumu

14Mar 2024
Na Mwandishi Wetu
Mara
Nipashe
Mwalimu Mkuu adaiwa kumlawiti mwanafunzi na kisha kumpa sumu

MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi  Masaunga wilayani Bunda mkoani Mara, Vicent Nkunguu (39) anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za kumbaka na kumlawiti mwanafunzi wa darasa la sita (16) na kisha kumnywesha sumu ili kupoteza ushahidi.

Akizungumza na chombo kimoja cha habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salum Morcase amesema vitendo vya ubakaji na ulawiti vilifanyika siku moja kabla ya kunyweshwa sumu siku iliyofuata.

Kamanda Morcase amesema mwanafunzi huyo alibakwa Machi 8, 2024 majiraya ya usiku akiwa amelala nyumbani kwa mtuhumiwa huyo Kijiji cha Kisorya alipokuwa amekwenda kwa ajili ya kuwapikia watoto wa mtuhumiwa baada ya kuombwa na mke wa mwalimu huyo aliyesafiri kwenda kwenye maombi katika Kijiji cha Igundu.

"Akiwa amelala na watoto chumbani, mwalimu huyo alikwenda kwenye chumba cha watoto na kumwambia mwanafunzi huyo kuwa, amekosa usingizi na kwenda naye kwenye chumba chake ambako alimbaka na kumlawiti," amesema.