Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Peter Majira, akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema tukio hilo limetokea Novemba 13, mwaka huu nyumbani kwa mchungaji huyo, John Mafwimbo, katika eneo la Sabasaba, Manispaa ya Singida.
Majira aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Michael Zacharia (54) Mkazi wa Utemini, John Damson (28) wa VETA na Samweli Sinda (30) wa Kibaoni katika manispaa hiyo.
Aliwataja walionusurika kuwa ni Mswede Malume (30), Ally Muka (26) na Emmanuel Damson (36) wakazi wa eneo la VETA.
Kwa mujibu wa Kamanda Majira, majeruhi hao walipelekwa katika Hospitali ya Rufani Mandewa na kuruhusiwa baada ya kupatiwa matibabu, hali zao zinaendelea vizuri.
Kaimu Kamanda huyo alisema uchunguzi wa awali uliofanywa na Jeshi la Polisi umebaini kuwa vifo na madhara kwa majeruhi hao, vimetokana na kuvuta hewa chafu iliyotokana na jenereta hilo walilokuwa wamelitumbukiza ndani ya karo kutoa moshi mwingi.
Katika tukio jingine; jeshi hilo linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kilo 13.
Majira aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Steven Ndege (24) na David Nelson (24), wakazi wa Mwanza.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika Hoteli ya Miami iliyopo Manispaa ya Singida baada ya polisi kupata taarifa kuwa walikuwa na dawa hizo kwa ajili ya kuzisafirisha kwenda mkoani Mwanza.
Alisema watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
"Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linatoa rai kwa wananchi kujishughulisha na shughuli halali ili kukipatia kipato halali na halitasita kumchukulia hatua kali mtu yeyote ambaye atatenda kinyume na sheria za nchi," alisema.
Vilevile amewataka wananchi kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha kuhakikisha usalama wao wanapokuwa katika shughuli zao ili kuepuka maafa yanayoweza kutokea.









