Watoto kuzaliwa kabla ya wakati ni mtihani mgumu

19Nov 2023
Godfrey Mushi
MOSHI
Nipashe Jumapili
Watoto kuzaliwa kabla ya wakati ni mtihani mgumu

ASILIMIA 20 hadi 25 ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) kisha kupoteza maisha 'wanawapasua vichwa' wataalamu wa Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) kutafuta namna ya kukabiliana na vifo hivyo.

Kati ya Januari hadi Novemba mwaka huu, watoto njiti 461 wamezaliwa KCMC huku idadi ya waliopokewa kutoka maeneo mbalimbali ni watoto 1,356.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufani ya Kanda ya KCMC, Prof. Gilleard Massenga, akizungumza wakati wa mapokezi ya vitanda vya kutunzia watoto waliozaliwa kabla ya wakati vilivyotolewa na Benki ya Maendeleo, alisema:

"Hili eneo la watoto njiti, yaani watoto wanaozaliwa kabla ya umri wao kufika wa kuzaliwa, ni eneo ambalo bado hatujafanya vizuri kama nchi na kama hospitali. Ni eneo ambalo kidogo linahitaji msukumo.

"Nitoe shukrani kwa wenzetu wa Benki ya Mendeleo kwa kutupatia vitanda tiba, ambavyo vitasaidia kupunguza vifo vya watoto hawa wachanga wanaozaliwa kabla ya muda wao.

"Hali halisi ilivyokuwa sasa hivi watoto wanaozaliwa kabla ya wakati wao kufika, nikiangalia takwimu za mwaka huu kuanzia Januari hadi sasa (Novemba), watoto njiti ambao wamezaliwa hapa KCMC ni watoto 461.

"Na tunavyofanya kutokana na utaalamu wetu asilimia 23 mpaka 25 bado hatuwezi kuokoa maisha yao. Kwahiyo, bado ni wengi ambao wanapoteza maisha. Tuseme mpaka asimilia 70 mpaka 75 tunaweza tukapambana nao, lakini wengine wanapoteza maisha."

Kwa mujibu wa Prof. Masenga, matatizo yanayochangia kupoteza maisha kwa watoto njiti ni pamoja na hali ya kuwa na joto la chini la mwili (Hypothemia).

Kabla ya makabidhiano hayo, Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo, Dk. Ibrahim Mwangalaba, alisema kati ya Sh. milioni 120 zilizokusanywa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kupitia Maendeleo Bank Marathon Februari 9 mwaka huu, Sh. milioni 60, zimetumika kununua vitanda kwa ajili ya kusaidia watoto wetu wanaozaliwa kabla ya wakati katika hospitali hiyo.

Kwa mujibu wa Dk. Mwangalaba, fedha nyingine Sh. milioni 60, zitatumika kukarabati majengo chakavu ya kituo kinachotunza watoto wenye usonji kilichoko Kurasini, Dar es Salaam. Kimepewa jina la Mtoni Diakonia.

"Sisi kama Maendeleo Benki tutaendelea kufanya kila lililo kwenye uwezo wetu kuhakikisha kwamba juhudi hizi kupitia Marathon zinadumishwa," alisisitiza Dk. Mwangalaba.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Jairy Khanga, ameeleza kuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanyika wa viashiria vya afya, ambao Rais Samia Suluhu Hassan aliuzindua hivi karibuni, Tanzania imepunguza vifo vya watoto wachanga kutoka vifo 25 kati ya vizazi hai 1,000 hadi vifo 24 kati ya vizazi hai 1,000.

Mkuu wa Idara ya Watoto na Daktari Bingwa wa Watoto KCMC, Dk. Aisia Shayo, alifafanua kuwa Hospitali ya KCMC, inapokea watoto waliozaliwa kabla ya wakati kwa idadi kubwa.

"Kwa mwaka jana, tulipokea watoto 1,356. Pia watoto hao asilimia chache, tuliwaruhusu kwenda nyumbani, ambao ni chini ya asilimia 50 kutokana na changamoto tulizokuwa nazo.

"Tunajitahidi kupubnguza vifo vyao na tumejitahidi kujielekeza kwa wenye uzito kati ya kilogramu moja, mpaka 1.5 kwa sababu hao unaweza kuwasaidia. Kwa wale chini ya kilogramu moja kamili inakuwa ni shida lakini bado tunajitahidi kuwasaidia," alisema.

BENJAMIN MKAPA

Jijini Dodoma, mwandishi wetu Renatha Msungu anaripoti kuwa asilimia 11 ya wanawake milioni mbili nchini hujifungua watoto kabla ya wakati kwa mwaka, huku sababu kubwa ikitajwa kuwa lishe duni.

Sababu zingine ni pamoja na ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu na maradhi mengine ambayo huwakumba wanawake.

Daktari Bingwa wa Watoto ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Watoto, Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Benjamin Mkapa (BMH), Julieth Kabengula, alibainisha hayo jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto Njiti Duniani.

Dk. Kabengula alitoa ushauri kwa jamii hususani wanawake kuandaa mwili kupokea mabadiliko ya ujauzito ili kuepuka kuzaa kabla ya wakati kutokana na hali hiyo.

Kuhusu watoto kuzaliwa utumbo ukiwa nje, bingwa huyo alisema hali hiyo inatokana na wanawake kuzaa katika umri mdogo kuanzia miaka 18 hadi 20 au kuzaa wakiwa na umri wa zaidi ya miaka 45.

Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Dk. Alphonce Chandika alisema wagonjwa ambao wamepata matibabu ya moyo kwa njia ya kufungua kifua na kutokufungua wameruhusiwa na wanaendelea vizuri.

Dk.Chandika alisema BMH alisema inaendelea kutoa matibabu ya moyo kwa wagonjwa na kusisitiza jamii iendelee kujitokeza kupata matibabu ya ugonjwa wa moyo katika hospitali hiyo.