Mkuu wa shule akatwa mapanga wakati akisimamia ujenzi wa shule

05Nov 2023
Sabato Kasika
Mara
Nipashe Jumapili
Mkuu wa shule akatwa mapanga wakati akisimamia ujenzi wa shule

MKUU wa Shule ya Sekondari Makojo, iliyoko Kijiji cha Makojo, Musoma mkoani Mara, Emmanuel Dagau, amenusurika kifo baada ya kucharangwa mapanga na mkazi wa kijiji hicho, Jaguji Musimo, akimtuhumu kuharibu eneo lake la kuchimba mchanga.

Mwalimu Dagau akiwa hospitalini akiwa amelazwa baada ya kukatwa mapanga. PICHA: SABATO KASIKA.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Julius Misana, akizungumza na Nipashe Digital kwa njia ya simu, alisema tukio lilitokea Jumatano, saa nane mchana, wakati mwalimu huyo akisimamia ujenzi wa bweni la shule yake.

Mwenyekiti huyo alisema mtuhumiwa anashikiliwa na vyombo vya dola, huku mwalimu akiwa amelazwa katika hospitali ya rufani ya Mwalimu Nyerere iliyopo mjini Musoma.

“Siku ya tukio mwalimu alikuwa anasimamia wanafunzi kusomba mchanga kwa ajili ya ujenzi wa bweni, lakini (mtuhumiwa) akadai kuwa ni kwenye eneo lake. Ndipo baadaye akamfuata mwalimu nyumbani kwake na kuanza kumshambulia kwa panga," alisema.

Alisema wanafunzi waliposhuhudia tukio hilo, walipiga kelele na (mtuhumiwa) akakimbia lakini polisi waliokuwa wakisimamia mtihani shuleni hapo walipopata taarifa walimfuatilia na kumkamata.

“Amefanya kitendo cha kutia doa kijiji chetu na kusababisha walimu kuogopa kuja kufundisha katika shule yetu wakihofia maisha yao,” alisema.

Panga lililotumika kumshambulia mwalimu.

Misana alisema mtuhumiwa huyo amemjeruhi mwalimu huyo sehemu mbalimbali za mwili ikiwamo na mikono na kumsababisha majeraha makubwa.

Mwenyekiti huyo alikanusha ya madai wanafunzi kuchota mchanga katika eneo mtuhumiwa kwa kuwa baada ya taarifa za tukio alifika kujiridhisha na kukuta sivyo kama alivyodai.

Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema kumekuwapo mtindo wa baadhi ya madiwani na wenyeviti wa serikali za vijiji kunyanyasa wafanyakazi, wakiwamo walimu jimboni mwake bila kuchukua hatua.

“Wafanyakazi wakiomba kuhama kutoka Musoma Vijijini tutawalaumu? Je, tunapolalamika kuhusu upungufu mkubwa wa wafanyakazi, tunajua tulisemalo?,” Profesa Muhongo alihoji wakati akizungumzia tukio hilo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Salim Morcase, alipotafutwa alisema tukio hilo bado halijafika ofisi kwake, mpaka afuatilie.