Aidha, imeelezwa gari hilo ni lenye namba za usajili T 307 CDH aina ya Ford Ranger lilikuwa kwenye kampuni ya kuuza magari ya CMC Automobiles Ltd kwa ajili ya matengenezo kutokana na kwamba lilikuwa bovu.
Hayo yalidaiwa na Meneja Utawala na Matengenezo kutoka Makao Makuu ya kampuni hiyo jijini Dar es Salaam, Ernest Msuya, mbele ya Jaji Edwin Kakolaki wakati akitoa ushahidi wa kumtetea Mrita anayetuhumiwa kumuua wifi yake huyo
Katika utetezi wake, alidai kuwa tarehe ambayo aliambiwa alikwenda nyumbani kwa wifi yake Kibada, Kigamboni kabla ya mauaji kutokea, gari hilo lilikuwa gereji kutokana na ajali ambayo ilikuwa imetokea wakati anarudi kutoka Nairobi kupeleka watoto shule.
Akiongozwa na Wakili Peter Kibatala, alidai kuwa gari hiyo tangu liuzwe na kampuni hiyo mwaka 2012 wao ndio walikuwa wanalifanyia matengenezo kwa sababu bado lilikuwa ndani ya waranti.
Alidai kuwa gari hilo liliuzwa katika tawi lao lililokuwapo Arusha na kwamba matawi yao yote yanafuata maelekezo kutoka makao makuu ndiyo maana yeye ana taarifa zote kuhusiana na gari hilo licha ya kwamba yuko Dar es Salaam.
Shahidi huyo, baada ya kupewa nyaraka (mwenendo wa gari) na Wakili Kibatala, aliitambua kuwa inatoka ofisini kwao Arusha ambayo ilitumwa jana na ikafika katika ofisi yao ya Dar es Salaam na kisha wakili akaichukua.
"Mheshimiwa Jaji naomba mahakama ipokee nyaraka ya mwenendo wa gari namba T 307 CDH aina ya Ford Ranger tangu mwaka 2012 kama kielelezo. Ina taarifa za lini gari liliingia kwa matengenezo na kutoka," alidai na kuomba.
Mahakama hiyo ilipokea kielelezo hicho na kuwa DE 11 kutokana na upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Paul Kimweri, kutokuwa na pingamizi.
Baada ya nyaraka hiyo kupokelewa, shahidi aliruhusiwa na mahakama kuisoma na kudai kuwa gari hilo lilirudi kwa matengezo katika kampuni yao kwa zaidi ya mara 10 na lilikuwa na tatizo la kugonga kwa injini.
Akifafanua baadhi ya tarehe, alidai kuwa Mei 15, 2016, Mei 18, 2016, Mei 20, 2016, Mei 23, 2016, Mei 25,2016 na Mei 26, 2016 gari hilo lilikuwa gereji katika kampuni hiyo kwa sababu lilikuwa bovu limerudishwa kwa matengezo.
Akiendelea kutoa ufafanuzi, Ernest alidai kuwa Agosti 10, 2016 gari hilo liliingia na kilometa 30,569 na lilitoka likiwa na kilometa 30,573, kwa hiyo lilizunguka kwa kilometa nne tun a hadi sasa bado liko CMC kwa sababu haliwezi kutembea.
"Walikuja askari polisi kutoka Arusha, wakataka kuchukua gari hili lakini wakaelezwa kwamba ni bovu na halina uwezo wa kutembea umbali mrefu. Polisi walilazimisha wakalichukua, hawakufika nalo mbali wakalirudisha,.
"Na kwa kitendo hicho walichokifanya mteja alikuwa hana taarifa wakati polisi wipokuja yaani kama yupo hapa basi ndiyo anayasikia haya kwa sababu ilikuwa ni kati yetu sisi na polisi," alidai Ernest.
Pia alidai kuwa kwa ubovu wa gari hilo, Mei 15,2016 hakukuwa na uwezekano wowote wa kutoka kutokana na ubovu lililokuwa nayo. Kwa kipindi chote hicho dereva ambae alikuwa akilipeleka gari hilo ni Karim Mruma.
Kwa upande wa mashitaka wanamtuhumu Mrita jkwamba Mei 15, 2016 alitumia gari namba T 307 CDH aina ya Ford Ranger kwa mara ya kwanza kwenda nyumbani kwa wifi yake, Aneth Msuya, kabla ya kabla ya kuuwawa Mei 25, 2016.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Jumatatu, ambapo jopo la mawakili wa Serikali litamuuliiza maswali ya dodoso shahidi Ernest kutokana na alichokizungumza mahakamani.
Miriam ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji ya wifi yake, Aneth, aliyeuawa Mei 25, 2016 kwa kuchinjwa shingoni nyumbani kwake, Kibada Kigamboni mkoani Dar es Salaam. Alikiri kuhusika na mauaji hayo katika maelezo yake ya onyo. Mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo ni Revocatus Muyela.










