Ummy alisema hayo jijini hapa, wakati akipokea ripoti ya tume huru ya uchunguzi wa malalamiko ya madaktari hao iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Prof. Mohammed Bakari Kambi.
Alisema ripoti iliyotolewa na tume hiyo imebaini kuwa malalamiko yaliyotolewa na madaktari hao hayana mashiko kwa kuwa uchunguzi umebaini hakuna aliyeonewa wala kupendelewa.
“Ndugu wanahabari, mtakumbuka kuwa niliunda tume hii mara baada ya kupokea barua ya malalamiko ya madaktari tarajali ambayo iliandikwa na kupelekwa kwa Mheshimiwa Rais na nakala nikapatiwa mimi.
“Tume hii imekamilisha uchunguzi wake na kubaini kuwa, wale ambao walifeli katika mitihani ile, walifeli kihalali na hakuna kuonewa kama ambavyo walivyokuwa wakilalamika katika barua yao,” alisema.
Waziri Ummy alisema kwa mujibu wa tume hiyo ambayo iliongozwa na Prof. Mohammed Kambi, aliyewahi kuwa Mganga Mkuu wa Serikali, ilifanya uchunguzi kwa kuhoji wadau mbalimbali.
Alisema licha ya kuhoji wadau mbalimbali, lakini pia ilipitia mitihani hiyo na kusahihisha upya na kubaini kuwa, wale waliofeli matokeo yalikuwa sahihi na hawakuonewa.
“Ninaagiza wote waolifeli warudie mtihani kwani sheria inawaruhusu kufanya mara tatu na atakayefeli awamu zote itabidi akasome upya mafunzo tarajali kwa miezi sita,” alisema.
Waziri Ummy aliagiza MCT kuendelea kuandaa mitihani hiyo kwa mujibu wa sheria.
Alisema lengo la mitihani hiyo ni kupima uwezo wa madaktari tarajali kabla kupatiwa leseni za kutoa huduma.
“Ninakubaliana na mapendekezo ya tume kuwa, mtihani huu ni jambo la muhimu sana ili kupata wataalam ambao watatoa huduma zisizokuwa na mashaka au malalamiko kwa jamii,” alisema.
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, alisema pamoja na uwapo wa mtihani huo, kuna haja kufanyika ukaguzi kwa vyuo vinavyotoa wataalam wa afya.
“Kwenye taaluma ya afya makosa hayaruhusiwi, ukimkosea kumtibu mtu unampa tiketi ya kifo au ulemavu wa kudumu tofauti nakada zingine kama sheria, mtu anaweza kukataa rufani,” alisema.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Prof. Kambi, alisema uchunguzi wa ripoti hiyo umefanyika kwa muda wa wiki tatu kwa kuhoji wadau mbalimbali wakiwamo walalamikaji na wasimamizi wa mitihani.
“Tulipatiwa wiki mbili kwa ajili ya kufanya uchunguzi lakini kutokana na ukubwa wa kazi hii tuliongeza muda wa wiki moja ambapo tulihoji wadau mbalimbali, kuandaa madodoso na kuhoji kwa njia ya mitandao kwa wale waliokuwa mbali,” alisema.










