Wabunge wataka vigogo ripoti CAG wanyongwe, wakatwe vichwa

05Nov 2023
Gwamaka Alipipi
DODOMA
Nipashe Jumapili
Wabunge wataka vigogo ripoti CAG wanyongwe, wakatwe vichwa

WABUNGE wametoa mapendekezo ya kunyongwa au kukatwa vichwa kwa viongozi wa serikali wakiwamo mawaziri na watumishi wa umma waliotajwa kuhusika na ufujaji wa fedha katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Wamesema ni wakati muafaka wa kuwasilishwa bungeni muswada na kutungwa sheria ya kutekeleza jambo hilo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia ya udokozi wa fedha za umma.

Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara, alisema ameshuhudia taarifa za CAG kwa zaidi ya miaka mitatu akiwa bungeni lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya wahusika wanaotajwa kuhusika na ubadhirifu.

Alisema kasi ya Rais Samia Suluhu Hassan kutafuta fedha ni kubwa lakini pia kasi ya wizi wa fedha za umma imekua kubwa sana.

Mwita alisema hatua hiyo ni sawa na Rais Samia anachota maji anaweka kwenye mkono wa kushoto lakini kuna watu wanatoboa pakacha, hivyo hayo maji hayawezi kujaa.

“Na mimi ninamapendekezo yangu, nchi kama Korea watu wanaokutwa na hatia ya ufisadi wananyongwa, sasa ninapendekeza waliodhibitika pasipo shaka bila ya kuwaonea wanyongwe, watoke katika nchi hii tubaki na watu wema,” alisema Waitara.

Alisema  Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imetoa mapendekezo mazuri, lakini yamepungua uzito.

“Mimi nilitarajia watuambie baada ya ripoti ya CAG wangapi wamefungwa? Wangapi wamefikishwa mahakamani? Wangapi wamefukuzwa kazi? wangapi wamerudisha fedha?. Pendekezo pekee ni kwamba iletwe sheria hapa watakaokutwa na hatia wanyongwe,” alisisitiza.

Mbunge wa Mbog’hwe (CCM), Nicodemus Maganga, aliunga mkono kuwapo kwa sheria ya kunyongwa kwa viongozi watakaobainika kuhusika katika ufujaji wa fedha ili kukomesha tabia hiyo.

“Ninaungana na (Mheshimiwa) Mwita kwenye sheria ya kunyongwa. Tuipitishe  hii sheria ili tuondokane na hii kitu. Kwa zaidi ya miaka mitatu nimekuwa nikiongelea suala hili, sasa ni wakati muafaka,” alisema Maganga.

Naye Mbunge wa Makambako (CCM), Deo Sanga, alisema: “Kupitishwa kwa sheria ya kunyongwa kwa viongozi watakaobainika na ufisadi, itapunguza tabia ya watu kuiba. Sheria iletwe hapa bungeni itasaidia watu kuogopa kuiba.”

Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole-Sendeka, alisema hatua ya kwanza ya kuondokana na vitendo vya ufisadi ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujitenga na watu hao.

Alisema mawaziri wanapaswa kujitenga na maofisa wanaohusika katika ufisadi kwa kuwaondoa na kuwaweka watu wengine ambao wanahofu ya kuiba.

Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Kilumbe Ng’enda, alisema matukio ya watu kufanya ubadhirifu wa fedha za umma yanaongezeka kila mwaka, hivyo ni wakati muafaka wa serikali kuleta muswada bungeni na kutungwa kwa sheria ya kunyongwa kwa watu hao au hata ikiwekezana kukatwa kichwa.

Mbunge wa Liwale (CCM), Zuberi Kuchauka, aliunga mkono hoja ya kutungwa kwa sheria kali ya kudhibiti vitendo vya ufujaji wa fedha, akisema itungwe ili iwe fundisho.

MBARAWA, NCHEMBA, KADOGOSA WATAJWA

Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina, alipendekeza Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, wakamatwe na kushtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi.

Mbunge wa Geita (CCM), Joseph Kasheku, alipendekeza wahusika wote waliotajwa katika ripoti ya CAG wapelekwe gerezani na wakafanye kazi za kulima hadi watakaporejesha fedha walizoiba.