Watu waliodaiwa kushambuliwa na Mtumbi ni Maneno Mathias (30), Paul Makonda (sio aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam) na Amina Sango anayedaiwa kuwa mpenzi wa marehemu.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo ambao hawakutaka kutajwa majina yao, walisema tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki, baada ya wenyeji waliompokea kumpatia eneo aliloomba kuchimba madini kwa ajili ya ujenzi.
Walisema siku aliyopewa eneo, alirejea alikofikia na kupata viburudisho na muda mfupi alianza kufanya fujo ikiwamo kukamata kuku na kumkata kichwa kwa kumng’ata kwa meno.
Mashuhuda hao walidai kitendo hicho kilimshangaza mpenzi wake na alipohoji, alimshushia kipigo, kilichomsukuma jirani yake Maneno Mathias (30) kuingilia kati.
Walidai kuwa wakati Mathias akijaribu kuamua mgogoro huo, Matumbi alichukua nondo na kumchoma tumboni na kupelekea kifo chake.
"Mathias baada ya kuchomwa na nondo tumboni alikimbia, lakini hakuwahi kufika alikokusudia na kuanguka chini na kufariki dunia," walidai mashuhuda hao.
Walisema kitendo cha Mathias kukimbia, Matumbi alimfuatilia baada ya kumkosa aliyemkusudia aliingia ndani ya nyumba anayoishi Makonda amejipumzisha, akamchoma nondo mgongoni, kiunoni na kumsababishia maumivu makali.
Mashuhuda hao walisema kitendo hicho kiliwachukiza wananchi ndipo walimshambulia kwa kutumia mawe na marungu na kufariki dunia.
Kamanda wa Polisi Mkoani Lindi, Pili Mande, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na watu hao kupoteza maisha huku mmoja akijeruhiwa.
Alisema Makonda amelazwa katika Hospitali ya Wilaya Liwale akiendelea na matibabu na kwamba hakuna anayeshikiliwa huku wakiendelea kuwasaka waliohusika.
MJAMZITO AUAWA
Wakati hayo yakiendelea Lindi, mkoani Geita vijana wawili wameuawa na wananchi wenye hasira kwenye Kitongoji cha Kilimahewa, Kata ya Ludete mkoani Geita baada ya kutekeleza mauaji ya mama mjamzito, Renatha Elias na kumjeruhi mume wake, Msafiri Renatus kwa kumchoma kisu sehemu mbalimbali ya mwili kisha kutaka kukimbia.
Inadaiwa kuwa mmoja wa vijana hao ni mwanafamilia na ni mtoto wa nje ambaye alifika na kijana mwenzake kwenye nyumba hiyo na kutekeleza mauaji ya mjamzito huyo wakati akiwa bafuni anaoga.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Marco Chuma, alisema aliyeuawa ni mama wa mji, mkuu wa kaya naye alipofika kwa ajili ya kupambana nao, alijeruhiwa kwa kuchomwa kisu maeneo mbalimbali ya mwili na kukimbizwa hospitalini.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Mgembe, aliyetembelea familia hiyo, alikemea matukio ya mauaji huku akiliagiza Jeshi la Polisi kuchukua hatua kali dhidi ya waliohusika.
"Kama una kijana au ndugu yako ambaye unafikiri anaweza kuendelea kutenda ujinga wa namna hii, mkanye mapema, hatutasita kumchukulia hatua stahiki za kisheria," alionya.
*Imeandaliwa na Said Hamdani (LINDI) na Vitus Audax (GEITA)










