...ikiwamo Shule ya Sekondari Thaqafa iliyoko jijini Mwanza na kufutiwa usajili wake kutokana na udanganyifu uliosababisha zaidi ya wanafunzi 300 kufutiwa matokeo ya mtihani huo.
Vilevile, imeagiza maofisa wote waliohusika kwenye udanganyifu huo wachukuliwe hatua kali ikiwamo kufukuzwa kazi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda aliagiza hayo jijini Mwanza jana alipokutana na wazazi wa wanafunzi 140 walifutiwa matokeo ya mitihani yao kwa kile kinachoelezwa walifanya udanganyifu kwenye mtihani huo.
Prof. Mkenda alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa baadhi ya walimu kwenye shule hizo walihusika kwa asilimia 100 kufanya udanganyifu huo kwa kuwafundisha majibu wanafunzi ili wakajaze kwenye mtihani huo wa taifa.
"Ushahidi tulionao kwa sasa sio wa mfanano wa majibu pekee, vilevile tunao ushahidi wa mwalimu ambaye alikuwa akiwafundisha majibu wanafunzi hao na wanafunzi wenyewe wamemtaja, hivyo hiyo inadhihirisha uhusika wa shule licha ya shule kuchukua hatua za kumfukuza mwalimu huyo ambaye tayari ametiwa mbaroni," alisema.
Prof. Mkenda alisema baada ya kutoa agizo hilo kwa Kamishna wa Elimu nchini, aliwataka wazazi wa wanafunzi katika shule hizo kuwaondoa mapema iwezekanavyo kabla ya shule hizo kufutiwa usajili wake, ili wanafunzi hao waendelee kupata elimu bila bughudha.
Alitaja shule nyingine ni za Sekondari Twiboke ya mkoani Mara na Memoric Academy Zanzibar.
Ufafanuzi wa serikali umekuja siku chache baada ya wazazi wa wanafunzi wa 140 wa Shule ya Sekondari Thaqafa jijini Mwanza kuandamana kwenye shule hiyo kujua hatima ya watoto wao huku wakihitaji kukutana na waziri mwenye dhamana awasaidie kutatua tatizo hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima, aliwataka wazazi kuzungumza na watoto wao kuhusu ukosefu wa maadili pindi wanapokuwa shuleni, ikiwa ni sehemu ya njia ya kudhibiti vitendo vya wizi wa mitihani sambamba na kupambana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.
Jumla ya wanafunzi 162 wa shule ya Sekondari Thaqaafa walifanya mtihani wa kumaliza kidato cha nne mwaka 2022. Kati yao, 22 matokeo yao yalitoka na 140 walifutiwa matokeo yao kwa kile kilichoelezwa walifanya udanganyifu kwenye mtihani huo uliofanyika Oktoba mwaka jana.
*Imeandaliwa na Neema Emmanuel na Vitus Audax










