Wimbo huo wenye maadhi ya Singeli na Mchiriku, ujumbe wake umewakanganya mashabiki wengi hasa wanawake walio katika ndoa.
Zuchu katika wimbo huo anasimama kama mwanamke mwenye tabia ya kuchukua waume za watu, na bila kupepesa macho anajisifia na kujitambulisha kwa kujiamini kwa mke wa mwanamume anayejivinjari naye kuwa yeye ni nyumba ndogo wake.
Maneno yaliyomo ndani ya wimbo huo kama vile kuhalalisha kimada au nyumba ndogo ni kama fasheni kwa wanawake, yameibua malalamiko kwa baadhi watu ambao wanasema ni kwenda kinyume na maadili ya Kitanzania.
Mwajabu Saidi, mkazi wa Temeke jijini Dare s Salaam, amesema licha ya wimbo huo kuwa mzuri, lakini ujumbe wake ndio wenye kuleta ukakasi, hasa kwa vijana wanaotamani kudumu katika ndoa zao.
“Zuchu ni msanii mkubwa na kila kitu anachokisema katika wimbo wake ni ujumbe tosha katika jamii, hili la kuhalalisha nyumba ndogo na kuonekana kama ni jambo la kawaida anaweza kuwapotosha wasichana wakiamini kuwa na mume wa mtu ni sehemu ya maisha,” amesema.
Amesema wanawake walio kwenye ndoa zao, wamekatishwa tamaa kutokana na wimbo huo wa Zuchu.
“Sijui kama watafurahishwa nao kuusikia, mume anauma sana si kama wasioingia kwenye ndoa wanavyofikiria” ameongeza
Christina Japhet, kwa upande wake amesema haoni tatizo na wimbo huo, kwani Zuchu ni msanii na anauwezo wa kuumba maneno ya kisanii ili kufikisha ujumbe wake.
“Mimi sioni tatizo wanaomkosoa watakuwa wanamuonea tu, unajua kila mwimbaji anatafuta maneno kwa ajili ya kupata mashabiki. Kusikifia nyumba ndogo si kama kapotoka kimaadili bali amekua kisanii na anaonyesha kipaji chake ya uimbaji,” amesema Christina.










