MultiChoice yatangaza mafunzo uandaaji filamu

12Jun 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
MultiChoice yatangaza mafunzo uandaaji filamu

KAMPUNI ya MultiChoice kwa kushirikiana na Bodi ya Filamu Tanzania, imetangaza rasmi fursa ya mafunzo ya uandaaji wa filamu kwa vijana wa Kitanzania kupitia programu maalum inayojulikana kama MultiChoice Talent Factory.

Programu hii ilizinduliwa rasmi Mei 2018 na imekuwa ikitoa mafunzo maalum ya uzalishaji filamu katika akademi maalum za MultiChoice Talent Factory Academy.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa kupokea maombi kwa awamu ya tatu, Mkuu wa Uhusiano MultiChoice Tanzania, Johnson Mshana, alieleza kuwa programu hiyo ni muendelezo wa programu maalum iliyodhamiria kuleta mabadiliko katika tasnia ya filamu barani Afrika.

“Baada ya miaka miwili ya mafanikio, MultiChoice inajivunia kutangaza awamu nyingine ya mafunzo ya uandaaji wa filamu kwa vijana wa Kitanzania wenye wito na masuala ya filamu.

"Tulianza kwa kupeleka vijana wanne katika akademi maalum kule Nairobi nchini Kenya Oktoba 2018, kisha vijana wengine wanne Oktoba 2019 ambao walihitimu mafunzo yao Aprili mwaka huu, na leo tunafungua rasmi dirisha la kupokea maombi kwa vijana wengine wa Kitanzania wenye wito na kazi za filamu kwa ajili ya darasa la mwaka 2022.

Maombi yote yatapokelewa kwa njia ya mtandao kupitia tovuti yetu ya https://cte.multichoicetalentfactory.com/Home/MTFHome. Na mchakato wa usajili utafanyika Julai hadi Agosti, mwaka huu na majina ya vijana watakaokidhi vigezo yatatangazwa mara baada ya mchakato kumilika ama kwa msaada zaidi namna ya kujiunga wasiliana na grace.mgaya@mutichoice.co.tz au simu namba 0765 065300," alisema Mshana.

Kwa upande wa Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dk. Kiagho Kilonzo, kwanza alipongeza Kampuni ya MultiChoice kwa kuwa mstari wa mbele katika kuleta mapinduzi kwenye tasnia ya filamu hapa nyumbani Tanzania.

“Binafsi ni shuhuda wa jitihada zinazofanywa na Kampuni ya MultiChoice katika kuhakikisha kwa pamoja tunaipeleka mbele tasnia hii na kufika katika viwango vya kimataifa.

"Hakika hii ni fursa ya kipekee kwa vijana wetu na ninapenda kuchukua nafasi hii kuwahamasisha vijana wote wenye wito na masuala ya filamu na sanaa kwa ujumla  kuitumia nafasi hii ipasavyo ili kuweza kujifunza, kubadilishana ujuzi na hatimaye siku zijazo nchi yetu iweze kupata waandaji wa kazi zenye maudhui ya hali ya juu,” alisema Dk. Kilonzo