Unaenda ukweni unasikia wanakuteta

22Jan 2024
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Unaenda ukweni unasikia wanakuteta

SIKU moja jamaa alikwenda ukweni, ambako shemeji zake wanaishi. Huko ndiko alikoolea.

Alikuwa anakwenda kupeleka pesa kiasi cha shilingi elfu 20 za mchango wa arobaini ya msiba uliotokea upande wa mkewe. Alipofika kabla hajaingia ndani akasikia wanaongea. Walichokuwa wakikiongea ndiyo alichoka mwenyewe. Walikuwa wanamteta yeye na mkewe. Yaani jamaa wanamsema mpaka ndugu yao.

"Yaani hata shilingi elfu 20 inawapelekesha hadi leo hawajatoa. Watu wote wametoa kasoro dada yetu tu na mumewe. Ndiyo basi tena imetoka hiyo. Wakilipa mimi siyo Pili." Jamaa alisikia wakiteta.

"Uliona hata kwenye msiba, yaani tunaitana kutoa hela, watu wanachanga, wao wanajivutavuta tu." Mwingine akadakia.

"Na dada yule mwanaume amempata wapi? Yaani hakuona wanaume wengine akamchukua yule. Mwanaume hajielewi, hana hela, wenzake wamekuja na magari pale, yeye na mkewe kwa miguu, hawana hata aibu, afadhali basi wangekodi hata bodaboda, wamekuja wameongozana kama kumbikumbi." Bado walikuwa wanaendelea kuwateta.

"Ndiyo maana kwenye msiba au tukikutana yeye ndiyo anatumwatumwa kwa sababu hana pesa, kapuku wa kutupwa, wenzake wamekuja na magari, utawatuma?"

Jamaa aliyasikia mwenyewe kwa masikio yake. Awali alidokezwa kuwa shemeji zake pamoja na kwamba wanaonekana wanampenda wanapokutana, lakini wanamchekea jino pembe tu.

Alichofanya ni kuingia ndani ghafla bila kupiga hodi. Shemeji zake ambao wote watatu walikuwa wa kike, walipomuona walishtuka na kuanza kujibaraguza.Halitaka kuwaficha, akawaambia kuwa walichokuwa wanaongea amekisikia. Ila hatojibu kitu na alichofuata pale ni kutoa pesa ya mchango arobaini ya msiba. 

Pamoja na kwamba wao walisema kuwa yeye na mkewe hawatolipa, wamefanya hivyo.  Akaiweka mezani, hakuaga akaondoka. Wakabaki wanaangaliana kila mmoja akishindwa hata kumlaumu mwenzake.

Mambo haya yapo sana kwenye jamii yetu. Wapo ndugu ambao wanasema wenzao kwa sababu tu wao wana uwezo na mwenzao hana.

Wanashindwa kutambua kuwa hata kama mkizaliwa kumi kwenye familia, siyo kwamba kila mmoja atakuwa na hali sawa na mwenzake.

Watatofautiana vipato, uwezo, vipaji, elimu na vitu nyingine vinavyofanana na hivyo.Hata kama ni watoto wa kike watapoolewa, wote hawawezi kuolewa na wanaume wanaofanana uwezo na kila kitu.

Sasa hii isiwe sababu ya wengine kuwadharau na kuwasengenya wenzao. Mungu anampa kila binadamu na riziki yake. Akimpa leo huyu kesho atampa mwingine.

Ndugu unayemcheka na kumdharau kesho ndiye atakayeikomboa familia hiyo hiyo wakati wengine wameshakula pesa zao, wamepata maraha sana na sasa wako hoi bin taaban.

Katika hili kikubwa ni kuwa pamoja na kusaidiana. Kwa nini wale wenye uwezo wasiwasaidie ndugu zao ambao hawana uwezo mkubwa badala ya kuwasengenya?

Hili nililolihadithia hapa lipo katika wimbo uliotwao 'Uteti', ambao ulipigwa mwanzoni kabisa mwa miaka ya 1980 na bendi ya UDA, iliyokuwa ikimilikiwa na Shirika la Usafiri Dar es Salaam (sasa UDAT).

Ulitungwa na mwanamuziki mwimbaji chipukizi wakati huo, lakini akaondokea kuwa staa mkubwa nchini, akipigia bendi mbalimbali kama Mwenge Jazz, DDC Mlimani Park Orchestra, Vijana Jazz Band. Huyu si mwingine bali ni Benovilla Antony.

Akiwa na bendi ya UDA Jazz ambayo ni kama ilimtambulisha kwenye ulimwengu wa muziki, alitunga kibao hicho kilichojichukua umaarufu mkubwa na kumfanya asikae sana katika bendi hiyo, akanyakuliwa na Mwenge Jazz, bendi inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Hebu pitia mashairi ya wimbo huu uone watu wenye tabia hiyo ambayo haikubaliki kwenye jamii.

"Siku moja nilipokuwa eee, natembelea kwa shemeji zangu, kitu kilichonishangaza sana njiani, ni kujiakwa kila mara.  Kabla  ya kuingia ndani nilisikia vicheko dirishani, nilisita kuingia ili nisikie kile kinachowachekesha. Kumbe ulikuwa uteti, kuhusu sisi mimi na ndugu yao, nilipoingia ghafla waliona haya, sikukaa nikaondoka.

"Muone haya, muone haya, muone haya, muone haya, mara nyingi nimeambiwa mwaniteta, na sasa nimesikia mimi mwenyewe, mara nyingi nimeambiwa mwaniteta, na sasa nimesikia mimi mwenyewe. Nicheke na nani, ooo na nani, niongee na nani, ooo na nani, iwapo ndugu zangu wenyewe mnanisengenya yoyoyoyo.

"Muone haya, muone haya, muone haya, muone haya, mara nyingi nimeambiwa mwaniteta, na sasa nimesikia mimi mwenyewe, mara nyingi nimeambiwa mwaniteta, na sasa nimesikia mimi mwenyewe. Mliyoyasema yote nimeyasikia, lakini mjue yote hayo mmetunga, hamkuanza leo kutusengenya wana wa wenzenu yoyoyo.

"Muone haya, muone haya, muone haya, muone haya, mara nyingi nimeambiwa mwaniteta, na sasa nimesikia mimi mwenyewe, mara nyingi nimeambiwa mwaniteta, na sasa nimesikia mimi mwenyewe."

Watetaji wamefumwa laivu, ni aibu kubwa, haikupaswa kuwa hivyo, huwezi kumteta ndugu yako mwenyewe badala ya kumsaidia.

Tuma meseji 0716 350534