SBL yatumia bia ya Guinness kuhamasisha sanaa ya uchoraji nchini

27Nov 2022
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
SBL yatumia bia ya Guinness kuhamasisha sanaa ya uchoraji nchini

Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) imeendelea kuhamasisha sanaa ya uchora kwa Watanzania kupitia bia yake ya Guinness, kwa kufanya shindano la uchoraji lililofanyika ukumbi wa Fuego Lounge, Jumamosi usiku.

Shindano hilo lililoitwa “Guinness Brews and Brushes” lilileta kwa pamoja, watumiaji wa bidhaa za SBL, wachoraji na wadau mbalimbali wa sanaa. 

Sanaa ya uchoraji imekuwa ikipanuka nchini Tanzania na kuvutia watu wengi sana hasa watalii na kuifanya Tanzania kuwa moja ya kituo cha sanaa ya uchoraji barani Africa.

Shindano hilo liliwata waalikwa wenye nia ya kujifunza kuchora au kipaji cha kuchora, kuonyesha uwezo wao na kusimamiwa na watalaamu wa Sanaa hiyo.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa SBL Rispa Hatibu alisema kuwa shindano hilo linahamasisha watu kukuza vipaji vyao vya kisanaa, hasa uchoraji.

“Tumeamua kuwapa watu nafasi ya kuonyesha vipaji vyao na kuwafanya waweze kung’ara kwa vile bia ya Guinness ina kauli mbiu yake inayowasihi watu kung’aa, hivyo tumefurahi kuwa hap ana kuona vipaji vipata nafasi ya kuonekana” alisema Rispa.

Mtangazaji maarufu wa Kituo cha Habari cha Efm, Bdozen, aliyekuwa mshehereshaji mkuu alisema ya kwamba Sanaa ni biashara na ni jambo jema kwa vipaji kukuzwa.

“Sote tunajua namna Sanaa inavyoweza kuwa na manufaa, kwa hiyo ni jambo zuri kwa Guinness kufungua mashindano haya ambayo mbeleni yanaweza kuza vipaji vya wachora wakubwa” Alisema. 

Mashindano hayo yawafanya baadhi ya wachoraji kuibuka washindi na kujishindia zawadi zilizoandaliwa na bia ya Guinness.