Kopa alisema hayo wakati akihojiwa na kituo kimoja cha redio, jijini Dar es Salaam na kufafanua kuwa kimya kingi kina mshindo mkuu, na kuwataka mashabiki wake kujiandaa kupata vitu vipya.
"Mashabiki wangu ninawaambia kuwa nipo, na wakati wowote nitatoa nyimbo mpya tano kwa pamoja, hivyo jiandaeni kusikia vitu vipya kutoka kwa Malkia wa mipasho," alisema Kopa.
Mbali na kufyatua nyimbo tano, mkongwe amewashauri wasanii wapya wa muziki wa taarab kuwa na heshima kwa wakubwa wao, kwa madai kwamba, bila kufanya hivyo hawawezi 'kutoboa' kwenye sanaa.
"Kila ninapokutana na wasanii wa kike huwa ninawashauri na kuwapa moyo kuhusu maisha ya muziki, kwani vijana wetu wengi wa sasa hivi hawana busara kusema ngoja nimfuate mtu mzima atanielekeza njia za kupita," alisema.
Kopa amesema wengi wanajifanya wanajua, hali ambayo hujikuta wakipotea mapema kwenye sanaa, huku yeye mkongwe akiendelea kufanya vizuri kwenye muziki huo hadi sasa.
Mkongwe huyo alitoa siri ya yeye kuendelea kudumu kwenye gemu kwa muda mrefu kuwa ni kutokana na kuongea vizuri na wale aliowakuta kwenye gemu na kupokea ushauri wao na kuufanyia kazi.
"Lakini leo mtu anaingia kwenye taarab tu na kuanza kupandisha mabega juu na kujifanya anajua kuliko wale aliowakuta. Kwa hali kama hiyo si rahisi msanii mchanga kutoboa, heshima ni ya muhimu," amesema.
Ameongezaa kuwa watu wengi huwa wanamuogopa, wakidhani kwamba ni mkali na kumbe ni wa kawaida na mtu poa, ambapo amewataka wale wanaohitaji ushauri kutoka kwake wamfuate bila hofu.