Huyo ndiye Misso Missondo kijana wa miaka 28 kutoka Masasi mkoani Mtwara, ambaye kwa sasa amekuwa habari ya mjini kwa uburudishaji kuanzia vituo vya redio hadi katika mitandao ya kijamii.
Pengine hakutarajia jina lake lingeweza kumaliza mwaka likiwa anga za juu na kusababisha watu kushindwa kupata usingizi kutokana na aina ya muziki wake wenye ladha adimu iliyochanganywa na ngoma za makabila mbalimbali.
Katika miezi michache hakuna aliyejaribu kulizima jina lake, na hata wale waliotaka kubadilisha upepo kwa kutambulisha wasanii wao, wamejikuta wakikumbwa na dhoruba kali la Misso Missondo na kujikuta wanacheza midundo yake bila kupenda.
Upepo wa Misso Missondo umemkumba kila mtu, ukiwa ndani ya daladala, bodaboda, bajaji na hata magari ya watu wazito utasikia ‘We Misso Missondo umepigaje hapo?
Hakika ni jambo la kumpongeza kijana huyu kutokana na ubunifu wake wa kuingiza muziki wa Singeli na ngoma za makabila mbalimbali, huku ikinogeshwa na wachezaji wake wazee wa masuti na kumfanya kila mtu kuwehuka.
Licha ya baadhi ya watu kujitokeza kumsaidia kusonga mbele, lakini serikali inatakiwa kumwona kwa macho makali ikiwa pamoja na kumwezesha kitaalamu ili kazi zake ziwe bora na zifike mbali.