Kwa mujibu wa meneja uhusiano wa bendi hiyo, wanenguaji hao ni Queen Suzzy aliyewahi kufanya kazi katika bendi ya Mashujaa Musica na Sabrina Mathew (pichani), ambaye aliwahi kufanya kazi bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta'.
"Hiyo ndio idadi ya wanenguaji ambayo tulikuwa tukiitaka ili wanapofanya kazi jukwaa liwe limeshiba kama ilivyokuwa miaka ya nyuma wakati tunazindua albamu ya kwanza ya Impact," alisema Pesambili.
Pesambili alisema bendi hiyo inajiandaa kwenda katika mikoa sita ya Kanda ya Ziwa Victoria kwenye kampeni za kupinga mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ikiwa imekamilika kila idara.
"Tuko hatua za mwisho za kukamilisha ratiba ya kwenda kwenye mikoa hiyo ya Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Mara, Geita na Kagera, tukiwa kamili ndio maana tukaongeza wanenguaji wapya wawili," alisema.
Bendi hiyo ina wimbo mpya uitwao 'Pinga Mauaji ya Albino, ambao utatumika katika kampeni hizo zinazotarajiwa kuanza wiki chache zijazo na zitakuwa za mwezi mmoja.










