Waziri aagiza wananchi kuunganishwa Faida Fund

16Jan 2023
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Waziri aagiza wananchi kuunganishwa Faida Fund

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama amezitaka taasisi zinazohusika na maendeleo ya vijana, wanawake na makundi maalum, kuanza kuhamasisha makundi hayo kuwekeza kwenye mfuko wa Faida Fund.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfuko huo uliopo chini ya Watumishi Housing mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Waziri Mhagama alisema serikali isingependa kuona Watanzania wanaachwa nyuma katika shughuli za uwekezaji na ukuzaji wa mitaji.

Waziri huyo alitoa pongezi kwa shirika la uwekezaji katika makazi la Watumishi Housing kwa kuja na ubunifu huo ambao si tu unatoa fursa ya wananchi kuwekeza kwa faida nzuri, bali pia unasaidia shirika hilo kupata mtaji wa utekelezaji wa miradi yake ya maendeleo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing, Dk. Fred Msemwa alisema uanzishwaji wa mfuko huo unatokana na maoni ya wawekezaji ambao wamekuwa wakipendelea kuwekeza mitaji yao kwa muda mfupi.

Dk. Msemwa alisema pamoja na mafanikio makubwa ya mfuko wa awali wa uwekezaji katika sekta ya makazi (WHC-REIT) uliozinduliwa mwaka 2014 na kukusanya zaidi ya Sh. bilioni 59, baadhi ya wawekezaji hususan wawekezaji binafsi wamekuwa wakiomba kuanzishwa kwa mfuko utakaotoa fursa kwa wawekezaji wengi zaidi.

"Kwa kuwa hili ni shirika la kizalendo, tuliazimia kuyafanyia kazi maoni ya wawekezaji wetu. Leo hii tunajivunia kuzindua mfuko huu wa uwekezaji wa pamoja wa Faida Fund.

"Mfuko huu haubagui kiwango cha chini cha uwekezaji hivyo unatoa fursa kwa mtanzania yeyote kujiunga," alisema Dk. Msemwa.

Mkurugenzi huyo wa Watumishi Housing aliishukuru Benki ya CRDB ambayo ni msimamizi wa mfuko huo pamoja na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali, kampuni ya sheria ya Abenry Advocates na Solomon Brokers kwa namna ambavyo wameshirikiana katika kuanzishwa kwa mfuko huo.

Akizungumza kwa niaba ya washirika wa mfuko huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela aliishukuru Watumishi Housing kwa kuipa benki hiyo fursa ya kuwa msimamizi wa mfuko huo na kubainisha kuwa benki hiyo imejipanga kuhakikisha Watanzania wote wanafikiwa na kunufaika na fursa hiyo.

Akielezea faida ya mfuko huo, Nsekela alisema ni wa kipekee kwa kuwa umezingatia sera mahususi ya huduma jumuishi za kifedha zinazomjali Mtanzania wa rika zote ikiwa ni pamoja na kununua vipande kwa Sh. 10,000, jambo ambalo linaenda sambamba na sera ya benki hiyo ya kuongeza ujumuishi wa kifedha.

Alifafanua kuwa mfuko wa Faida Fund unakuwa mfuko wa saba katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja. Alisema benki hiyo imejipanga kusimamia mfuko huo kikamilifu na kuhakikisha maslahi ya wawekezaji yanalindwa.

Nsekela alimweleza Waziri Mhagama kuwa benki hiyo inajivunia kuwa kinara katika huduma bora za uwekezaji katika masoko ya mitaji. Alibainisha kuwa Benki ya CRDB inachangia zaidi ya asilimia 70 ya wateja wote wanaoshiriki katika masoko ya mitaji na dhamana.

Mwaka jana Benki ya CRDB ilitunikiwa tuzo na Soko la Hisa la Dar es Salaam kwa kuitambua benki hiyo kama kinara wa huduma bora kwenye masoko ya mitaji.

Benki hiyo inatoa huduma ya kuuza na kununua bidhaa zote za masoko ya mitaji kupitia mtandao wa matawi yake kote nchini.