Katika utekelezaji wa mradi huo, Wizara ya Kilimo inasimamia eneo la kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi na halmashauri ya wilaya ni mtekelezaji wa shughuli za mradi. Mradi huu kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ulianza kutekelezwa mwaka wa fedha 2019/20.
Mradi unatekelezwa kwenye vijiji vitano vya Melela, Magali, Lukenge, Mingo na Lubungo ambapo utekelezaji huu ulizingatia mgawanyiko wa kiikolojia katika wilaya huku ukielekezwa zaidi kwenye maeneo yenye asili ya uhaba wa mvua na yakiwa yameathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi kutokana na shughuli za kibinadamu na majanga ya asili. Uchaguzi wa vijii hivyo ulitokana na utafiti uliofanyika ambapo vijiji hivyo vilikidhi haja ya mradi.
Shughuli za mradi katika Wilaya ya Mvomero zilikubalika baada ya kuibuliwa na wananchi wanufaika katika vijiji mwaka 2019 ambazo ni pamoja na uchimbaji wa visima (4) kwa ajili ya shughuli za kilimo, mifugo na matumizi ya majumbani, uchimbaji wa lambo (1) kwa ajili ya kuvuna maji kwa shughuli za kilimo, mifugo na majumbani, ujenzi wa mfereji mkuu wa umwagiliaji katika skimu ya Lukenge na uenezaji wa teknolojia ya matumizi ya majiko banifu na matumizi ya nishati mbadala.
Shughuli nyingine zilizoibuliwa ni uanzishwaji wa mashamba darasa ya kitalu nyumba (4), uboreshaji wa mbuzi wa maziwa, ujenzi wa josho (1) la kuogeshea mifugo, uanzishwaji wa vikundi vya uzalishaji katika vijiji, uopoaji wa maeneo yaliyoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na ujenzi wa kituo cha kukusanyia maziwa.
Mabadiliko ya tabianchi yamesababisha uhaba wa unyevu katika mabonde yaliyokuwa yakitumiwa na wananchi kwa shughuli za kilimo na ufugaji kipindi cha kiangazi.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Mratibu wa Mradi wa EBARR Wilaya ya Mvomero, Baraka Mteri anasema mradi umetumia mbinu ya kiikolojia ya matumizi ya maji yaliyomo ardhini (uchimbaji wa kisima) ambapo yatawezesha shughuli za kilimo na/au mifugo kuendelea hata kipindi cha kiangazi na hivyo kuwa suluhisho la upatikanaji wa unyevu (maji) kwa shughuli za uzalishaji.
Kazi ya uchimbaji wa visima katika Kijiji cha Mingo na Magali imekamilika na kwa sasa wananchi wanachota maji kwa matumizi ya majumbani na wengine wakiendesha shughuli zakilimo kwa kutumia maji hayo.
Mteri anasema lengo la kuchimba visima hivyo ni kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi yaliyopelekea maeneo ya mabondeni walikokuwa wanalima wananchi hao kukauka na sasa kuwa eneo kame, hivyo wao kushindwa kuzalisha mazao ya mboga kama walivyokuwa wanazalisha zamani.
Anasema mradi wa visima virefu unanufaisha wananchi takribani 1,350 katika vijiji vya Magali na Mingo. Jumla ya hekta 78 zitamwagiliwa na kuzalisha mboga kwa kutumia maji ya kisima.
Moja kati ya teknolojia inayoaminika kufanya vizuri katika afua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, ambapo matumizi sahihi na bora ya maji ni mojawapo ya afua za kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi.
Mteri anasema kwa kutambua hilo, mradi umewezesha ujenzi wa mfereji mkuu wa umwagiliaji katika Skimu ya Lukenge ambayo tangu mwaka 2012 ilipojengewa banio na miradi ya ASDP1 hakukufanyika ujenzi wa mfereji.
"Kwa sasa ujenzi wa mfereji umefikia mita 1,200 kati ya 2,750 huku kigawa maji namba moja kikiwa kimekamilika na kina uwezo wa kumwagilia hekta 125. Mradi wa umwagiliaji ukikamilika utanufaisha wananchi 3,100," anasema.
Katika kueneza teknolojia ya matumizi ya majiko banifu na matumizi ya nishati mbadala, Mteri anasema jumla ya majiko banifu 595 yametengenezwa katika vijiji vinavyotekeleza mradi huu (Melela 170, Lubungo 137, Mingo 141 na Magali 147 kati ya majiko 460 yaliyokuwa yanatarajiwa kujengwa ili kupunguza msukumo wa matumizi ya misitu kwa nishati ya kuni.
Anabainisha kuwa jumla ya miti 86,479 inaendelea kutunzwa katika mashamba ya wananchi wa vijiji hivyo.
"Kwenye eneo hilo mradi umekwishawezesha vikundi kadhaa vya ufugaji wa nyuki- Lubungo, utengenezaji wa sabuni na uzalishaji wa uyoga. Mpaka sasa jumla wanavikundi 78 wananufaika na miradi hii," anasema.
EBBAR (Ecosystem-Based Adaptation for Rural Resilience in Tanzania) ni mradi unaopaswa kutunzwa na kuhakikisha unakuwa endelevu kwa kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zitaendelea kuwapo, hivyo uendelevu wa miradi inayotekelezwa na mradi huu na miradi mingine inayofanana na hii ni muhimu kusimamiwa na kuendelezwa ipasavyo.










