Wamesema bei ya sukari kutoka kwenye mataifa hayo inauzwa kwa bei ndogo kuliko ya Tanzania, lakini wakitaka kuinunua wanakutana na vikwazo vya kiforodha ambavyo wakivitekeleza bado bei inakuwa juu.
Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti mwishoni mwa wiki, baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Mbeya wamesema bidhaa hiyo imeadimika na hata inayopatikana ni kidogo, inauzwa kwa bei ya juu ambayo wanashindwa kuimudu.
Mmoja wa wananchi hao, Mariam Mwakibasi mkazi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi ambaye pia ni mama lishe alisema awali walikuwa wananunua sukari kwa Sh. 2,500 na 2,800 lakini kwa sasa wananunua kwa Sh. 4,500 na 5,000 bei ambayo amesema haijawahi kupanda kwa kiwango hicho.
Amesema kutokana na kupanda kwa bei hiyo hata wao wamelazimika kupandisha bei ya bidhaa zinazotokana na sukari ikiwemo mandazi, chapati na chai, hali ambayo imesababisha kuanza kukosa wateja.
Amesema kwa sasa sukari ya kutoka Malawi na Zambia imeanza kuingia kwa njia za magendo, lakini bado haziwasaidii kutokana na waingizaji kuuza kwa bei inayokaribiana na ya Tanzania.
“Maandazi ambayo tulikuwa tunauza Sh.200 sasa hivi tunauza Sh. 300, chapati tulikuwa tunauza mbili kwa Sh. 500 sasa hivi chapati moja tunauza Sh. 300 na wengine wanauza Sh. 400 mpaka Sh.500, sasa ni kitu ambacho wateja wetu hawajazoea na hivyo wameanza kutukimbia,” amesema Mariam.
Jailos Kijalo amesema sukari kutoka Malawi na Zambia zinauzwa maeneo ya mipakani kwa kati ya Sh. 2,500 na 2,700 lakini haziruhusiwi kuingizwa nchini bila kulipiwa ushuru hali ambayo inasababisha bei ya bidhaa hiyo kuendelea kuwaumiza wananchi.
Amesema anafanya biashara zake kati ya Mji wa Tunduma, Jiji la Mbeya na Kyela lakini amekuwa akishuhudia maofisa wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) wakiwakamata wananchi wanaosafirisha sukari ya Malawi na Zambia kupeleka Mbeya.
Amesema maofisa hao huwa wanaingia kwenye magari ya abiria na kukagua na kwamba wakiikuta sukari hiyo wanataifisha na wakati mwingine wanamchukulia hatua mwenye gari.
“Sasa hivi sukari za Zambia na Malawi zinauzwa kama bangi, wafanyabiashara wanauza kwa kificho japo ndiyo inasaidia watu, sukari yetu haipatikani kabisa na hata ukiipata unaunua kwa bei ya juu sana, kwahiyo binafsi nashauri serikali ilegeze masharti ya uingizaji wa bidhaa hii kutoka nchi hizi jirani,” amesema Kijalo.
Mmoja wa wafanyabiashara wa Jiji la Mbeya ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema kwa sasa sukari ya Tanzania inauzwa kwa bei ya kati ya Sh.95,000 na Sh.100,000 kwa katoni yenye uzito wa kilogramu 20 na kwamba pamoja na bei hiyo bado haipatikani.
Amesema wafanyabiashara wakubwa wanauza bidhaa hiyo kwa kificho na kwamba kama hawajakuzoea hawauzi hali ambayo inasababisha bidhaa hiyo kuendelea kuadimika.
“Hata mimi nikiipata kwa bei hizo nalazimika kuuza Sh.5,000 ili angalau nisiwapoteze wateja wangu, kwa sasa sukari kwangu siyo biashara kwa sababu sipati faida yoyote na wakati mwingine huwa naona bora nisiwe nayo ili kuepuka sheria kwa sababu tunawindwa,” amesema mfanyabiashara.
Kwenye Kikao cha Ushauri cha Mkoa wa Mbeya (RCC) kilichofanyika mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Mkoa huo, Juma Homera ameagiza wakuu wa wilaya mkoani hapa kusimamia bei elekezi ya sukari kwenye maeneo hayo kwa kuhakikisha haiuzwi kwa zaidi ya Sh. 3,000.
Pia amewataka kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wafanyabiashara ambao wanauza bidhaa hiyo kwa bei ya kuruka akidai kuwa ipo sukari iliyoingizwa mkoani humo na Bodi ya Sukari Tanzania (CBT).
Sukari imekuwa tatizo nchini kutokana na upatikanaji wake kuwa mdogo na hata inayopatikana inauzwa kwa bei ya juu ambayo inaumiza wananchi.










