Kutokana na tatizo hilo Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya, Suma Fyandomo amekabidhi madawati 30 ili kupunguza tatizo hilo.
Akizungumza wakati akikabidhi msaada huo, Fyandomo amewataka wadau mbalimbali wa maendeleo kusaidia maeneo yenye matatizo kwenye sekta ya elimu ili kuiunga mkono serikali kutokana na maendeleo ambayo inayafanya.
Fyandomo amesema pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali katika kuimarisha sekta ya elimu nchini, wadau mbalimbali wana nafasi ya kuunga mkono jitihada hizo kwa kutatua kero mbalimbali ikiwemo upungufu wa madawati.
“Serikali imeweka elimu bila malipo ili kuhakikisha watoto wetu wote wanapata haki yao ya kielimu na kutimiza ndoto zao, hivyo ni muhimu na sisi tukachangia kutatua hizi kero ambazo ziko ndani ya uwezo,” amesema Fyandomo.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Thomas Mwanga, amesema halmashauri hiyo ina mikakati ya kushirikisha wadau mbalimbali katika kuhakikisha tatizo la upungufu wa madawati linaisha.
Amemshukuru mbunge huyo kwa kuchangia madawati hayo na kuwataka viongozi wa shule hiyo kuhakikisha madawati hayo yanatunzwa vizuri ili yaweze kutumika kwa muda mrefu.
Diwani wa Kata ya Mpuguso, Japhet Mwakagugu, amesema madawati yaliyotolewa yamewapunguzia mzigo wa upungufu uliokuwepo na kuwataka wananchi wa kata hiyo kuwaunga mkono viongozi na wadau mbalimbali wanaojitoa kuchangia maendeleo.










