Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. John Jingu, alitoa agizo hilo jijini hapa alipofanya ziara ya kikazi kwenye Hospitali ya Rufani ya Mkoa Dodoma, iliyolenga kukagua utendaji kazi na kuzungumza na watumishi wa hospitali hiyo.
Katika ziara hiyo aliambatana na Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu na Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk. Best Magoma.
Amesema watoa huduma wanapaswa kuwa na weledi wenye kutumia lugha nzuri za staha pamoja na kulinda na kuzingatia haki za wagonjwa.
“Ni jukumu la kila mtumishi kuwahudumia wagonjwa sawa sawa kwa sababu tunategemea kila anayekuja kupata huduma ni mgonjwa, hivyo huenda akawa na hasira ila unatakiwa kumuhudumia na kumpokea vizuri na nilitoa maelekezo kwa hospitali zetu zote kuanzishwa kwa dawati la kusikiliza maoni, kero na malalamiko ya wateja ambalo linaonekana na kufikika na watoa huduma muda wote na wenye weledi na watakaokuwa na lugha za staha zinazozingatia mila na desturi zetu za kitanzania ikiwamo kutunza siri za wagonjwa,” amesema.
Pia amewahimiza watumishi katika sekta ya afya nchini kufanya kazi kama timu na kudumisha ushirikiano ili kuzidi kuimarisha na kuongeza ufanisi na tija katika utoaji wa huduma bora kwa Watanzania.
Dk. Jingu alipongeza watumishi wa hospitali hiyo kwa ubunifu wa utoaji wa huduma bora na nzuri wagonjwa, usafi wa mazingira ya hospitali na ushirikiano walioutoa wakati wa janga la maporomoko ya Wilaya ya Hanang.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Tumaini Nagu, alipongeza kwa huduma bora zinazotolewa na watumishi wa hospitali hiyo hasa katika huduma za uzazi.
Hivyo aliwataka watumishi kuzidi kuongeza umakini na kuwapo kwa miongozo na taratibu ya utekelezaji wa majukumu yao katika vitengo vyote vya kutolea huduma ili kupunguza makosa ya kitabibu.









