Katibu Mkuu huyo, amesema hayo wakati akifungua Kikao kazi cha Makatibu Tawala wasaidizi Elimu mikoa na Maofisa Elimu wa Halmashauri nchini mjini Morogoro
Amesema licha ya dhamira njema ya serikali ya kutekeleza miradi mbalimbali ya elimu, wapo baadhi ya viongozi ambao wameshindwa kusimamia na kukamilisha utekelezaji wa miradi hiyo kwa muda uliopangwa.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi ametolea mfano kuwa ipo mikoa ambayo ujenzi wa miundombinu ya shule bado ipo chini ya asilimia 50, licha ya maelekezo ya serikali ya kuwataka kukamilisha ujenzi kabla ya Desemba 30, 2023.
“Lazima mjue kuna walio kamilisha miradi hiyo huku wakiwa na mazingira magumu kuliko nyie mnaosuasua “alisema Katibu mkuu Tamisemi Ndunguru bila kuitaja mikoa hiyo.
“…Katika hili nikiwa Afisa Nidhamu na Ajira kwenu sitaona haya kuchukua hatua kali kwa wachache wanaotukwamisha katika ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu ya shule pamoja na afua nyingine za miradi” alionya Ndunguru.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi, ametoa maagizo kwa Makatibu Tawala wasaidizi elimu mikoa kwa kuwataka kusimamia kikamilifu ufundishaji na ujifunzaji shuleni na kuhakikisha walimu wasiotimiza wajibu wao wanachukuliwa hatua stahiki.
Pia amezitaka kila halmashauri nchini kusimamia utekelezaji wa mpango wa mafunzo endelevu ya walimu kazini (MEWAKA) na kuhakikisha mafunzo hayo yanachangia ufanisi katika ufundishaji na uendelezaji.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi ,amewasisitiza wajenge tabia ya kuwatia moyo na kusikilizwa walimu badala ya kuwakatisha tamaa, ikiwa na kuacha kutumia lugha za udhalilishaji kwao .
Naye Naibu Katibu Mkuu Tamisemi anayeshughulikia sekta ya Elimu, Dk. Charles Mdonde amesema utekelezaji wa mkakati wa uboreshaji elimu umeanza kuzaa matunda kwa kuonesha takwimu za watoto waliopimwa kila kota (Machi 2023) kwa darasa la kwanza walijua kusoma, kuandika na kuhesebu.










