Malalamiko hayo wameyatoa mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Njombe.
Kamati hiyo ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka ilifika kijijini hapo kwa lengo la kusikiliza kero za wakazi hao katika mkutano wa hadhara.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi hao walidai kuwa viongozi wa kijiji hicho wamekuwa wakiongeza fedha kwenye michango wanayokubaliana kwenye mikutano ya kijiji.
Walidai wakati mwengine mgambo wanapita nyumba kwa nyumba kudai michango na kama mwanakijiji hana, wanamshushia kipigo na kuingia ndani na kumwamgia maji magodoro na nguo kama njia ya kushinikiza kulipwa fedha.
Mmoja wa wakazi hao, Jafari Mnenwa alisema awali walikubaliana kuchanga fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, kabla hawajakamilisha hilo viongozi wa kijiji hicho wakaja na michango mingine.
“Tuna mpango wa kujenga madarasa kabla hatujamaliza kujenga tunachangishwa fedha kwa ajili ya kununua uwanja kwa ajili ya kujenga ofisi ya kijiji,” alisema Mnenwa.
Mnenwa alisema pia katika mikutano yao walikubaliana atakayechelewa kutoa mchango atamlipa mgambo Shilingi 5,000 badala yake wamekuwa wakitoza Shilingi 10,000.
“Tulikubaliana kama ukichelewa utatoa faini Shilingi 5,000 ambayo ni ya mgambo lakini cha kushangaza wakifika wanakulazimisha utoe Shilingi 10,000 na usipotoa wanakupiga, tumechoka na haya manyanyaso,” alilalamika Mnenwa.
Mnenwa alisema amekuwa akifuatilia changamoto kijiji hapo na kuhoji lakini matokeo yake ameishia kubambikiwa kesi ya wizi wa sola ambayo alinunua Shilingi 160,000.
Elida Ndalagwa alisema: “Mimi ni mjane mashamba yangu yamevamiwa na ndugu wa mume wangu, ambao wanalima pale lakini wakaenda polisi kunishtaki nimewatishia na panga, nikakamatwa nikapelekwa Kituo cha Polisi Ilembula nikalala mahabusu kulikuwa na askari polisi wawili wa kike na wa kiume wakanichukulia hela zangu 150,000.”
Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Wangutwa, Ester Mrunwa alisema katika mkutano wa hadhara walikubaliana kila mwakajiji kuchangia Shilingi 5,000 kwa ajili ya kununua kiwanja.
Ester alisema katika mkutano huo walipeana muda kuwa atakayechelewa atakamatwa na kulipa kwa mgambo Shilingi 10,000.
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Wanging’ombe, Magnus Milinga alisema walipata taarifa kwamba Jasari anazo mali za wizi na kuchochea uvunjifu wa amani.
“Baada ya kupata hiyo taarifa tulikuja kupekua na baadhi ya mali na ambazo tulijua ni mali yake halali tulimkabidhi, tulimkuta na sola pamoja na pikipiki ya wizi,’’ alisema Milinga.
Kufuatia malalamiko hayo, Mtaka alipiga marufuku kuwepo michango kwa sasa hadi wananchi hao wanatapokubaliana upya.
“Mheshimiwa diwani naomba hii michango isimame hawa watu walime, wafanye shughuli za mavuno na wakivuna mtakaa sasa mkubaliane shughuli za maendeleo mnafanyaje,” alisema Mtaka.