Malalamiko hayo yalitolewa na wawekezaji wa kiwanda hicho wakati wa ziara ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya ya kutembelea viwanda mbalimbali mkoani hapa kwa lengo la kusikiliza kero zao na kukagua mwenendo wa uendeshaji.
Meneja uzalishaji wa kiwanda hicho, Lameck Elias alisema Julai mwaka jana kuna watu walivamia kiwandani hapo na kuiba mabelo 70 ya mifuko na na kuwasababishia hasara.
Alisema walitoa taarifa polisi kuomba msaada wa kuwasaka watuhumiwa na kufanikiwa kuwakamata na kutakiwa kurejesha mifuko hiyo.
Alisema watuhumiwa walirejesha mabelo hayo ambayo hayafiki hata nusu ya yale yaliyokuwa yameibwa na yaliyobaki imekuwa kizungumkuti na kuzua wasiwasi kwa kiwanda hicho.
“Polisi walituahidi wanalishughulikia lakini mpaka sasa wako kimya, sasa tunashindwa kuelewa kwa nini maana wahusika walikamatwa na wakarejesha mabelo mengine,” alisema Lameck.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera aliliagiza jeshi hilo kushughulikia tatizo hilo haraka kwa kuhakikisha watuhumiwa hao wanarejesha mifuko yote waliyoiba ili wawekezaji hao waendelee kufanya kazi kwa amani.
Homera alisema kama watuhumiwa walikamatwa hakuna sababu kwa jeshi hilo kushindwa kuwalazimika kurejesha bidhaa hizo.
“Kama wahusika walikamatwa na wakarejesha karibia nusu ya mabelo hayo, inashindikanaje maabelo yaliyobakia kutorejeshwa,” alihoji Homera.
Aliliagiza jeshi hilo kushughulikia kero hiyo ndani ya wiki moja ili wawekezaji hao waendelee na shughuli zao za uzalishaji bila kikwazo.
Akimwakilisha Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ofisa Polisi Jamii wa Mkoa huo, George Salala alisema tatizo la wizi kwenye viwanda kikiwemo hicho lipo.
Alisema wamekuwa wakishirikiana na wawekezaji kuhakikisha matukio ya aina hiyo hayatokei na kwamba tukio la wizi uliotokea kwenye kiwanda hicho aliwahi kulisikia na kuahidi kufuatilia ili mwisho wake ujulikane.
Alisema baada ya kulifuatilia watatoa taarifa ndani ya muda mfupi kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huku akisisitiza kuwa watahakikisha maeneo yote ya wawekezaji yanakuwa salama.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya pia ilitembelea Kiwanda cha Saruji cha Songwe na viwanda vya vinywaji vikali na baridi vilivyopo Iyunga jijini Mbeya.










