Wakulima walia mfumo ugawaji mbolea

08Oct 2022
Na Mwandishi Wetu
SAME
Nipashe
Wakulima walia mfumo ugawaji mbolea

WAKULIMA wadogo wameiomba serikali  kufuatilia kwa karibu ugawaji wa mbolea ya ruzuku ambao katika baadhi ya maeneo umegeuka maumivu kutokana na mfuko wa kilo 50 kuuzwa zaidi ya Sh.120,000 badala ya bei elekezi ya Sh. 70,000.

Aidha, wamesema makundi maalum hayapati mbolea hizo huku anayehitaji kuanzia kilo moja kuendelea hawezi kupata hadi aununue mfuko mzima wakati uwezo wake ni mdogo.

Madai hayo yalitolewa jana na wakulima kutoka wilayani Mbeya na Hai, mkoani Kilimanjaro, wanaoshiriki Tamasha la Jinsia Kanda ya Kaskazini lililoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), lililomalizika jana wilayani hapa.

Hobokela Kilindu, mkazi wa kata ya Tembela mkoani Mbeya, alisema mbolea ya ruzuku ni maumivu makubwa kutokana na masharti yaliyowekwa ambayo kwa mtu mwenye ulemavu au mzee hawezi kuzipata kwa urahisi na kwa wakati kwa kuwa wengi wanasema hawana vocha (ruzuku ya serikali) hadi baada ya wiki moja.

“Anaweza kukwambia lete fedha alafu baada ya siku tatu au nne ufuate mbolea. Mkulima nina malengo yangu unahitaji ila unakosa kwa sababu mawakala si waaminifu. Huwezi kupata mbolea kwa Sh. 70,000 lazima uongeze fedha hadi Sh. 90,000 na unaenda kuifuata  kilomita mbili au zaidi,” alisema.

“Unapofika kwa wakala kuna vijana ambao sielewi wameajiriwa na nani. Hata  kama una uwezo wa kupakiza kwenye gari mwenyewe lazima uwalipe hao vijana wakupakilie kila mfuko Sh. 500 na wanakwambia wazi bila hawa hupati mbolea, bado usafiri kutoka kijijini hadi kwa wakala,” aliongeza.

Aidha, Kilindu alisema mfumo wa sasa umeondoa wauzaji wadogo ambao wanatakiwa wawe wasomi, uwe na leseni na cheti cha ufaulu ndio wauze viuatilifu na mbolea.

“Walikuja Mbeya wakafundisha watu wakatoa mtihani kwa waliofaulu walipewa vyeti, wakaondoka kwa uliyesoma kama hujafaulu unahama kwenda mkoa mwingine ili ufanye mtihani uwe wakala, hili ni tatizo kama huna ada ya Sh. 300,000 huwezi kusoma na kuwa wakala, hii imeua ajira zetu,” alisema.

Kilindu aliishauri serikali ifanye tathimini na kuangalia upya huu mfumo, ingeacha mfumo wa zamani au mawakala wawape elimu ya kutosha kwa sasa wamekuwa miungu watu.

“Nia ya serikali kuleta mapinduzi ya kilimo haitafikiwa mfano eneo letu muda wa kupanda umefika na mbolea hakuna, wanatengeneza mazingira ili ipande bei. Mbolea ya ruzuku inatakiwa Sh. 70,000 lakini hadi sasa ili upate haraka ni 90,000 na nyingine 80,000 hadi 100,000 bado hujaweka usafiri.

“Tunatoka mbali sana unapanda basi kutoka Tembela hadi Mbalizi, kama unaenda kuchukua mfuko mmoja unatumia 10,000 hadi 15,000,” alifafanua.

Naye Janeth Barnaba mkazi wa Kata ya Mbalizi, Mbeya,  alisema wenye ulemavu na wazee wanapata tatizo kupata ruzuku hiyo kutokana na umbali kutoka kijijini hadi kwa wakala.

“Mzee au mlemavu anaandikishiwa Mshewa alafu anatakiwa kusafiri hadi Sido Mbeya mjini kuweka dole gumba alafu atatakiwa kwenda Mbalizi anatumia nauli ya Sh. 8,000 kwenda na kurudi, akikutana na dalali amlipe 20,000 hivyo anaipata mbolea kwa zaidi ya Sh. 100,000 bado hatujawasaidia wakulima kabisa,” alisema.

Naye Mkulima na Mjasiriamali wa wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, Etropia Assenga, alisema eneo lao kuna utaratibu wa kujiandikisha kwa kata na vijiji, kwa mabalozi kupita kila nyumba ambao wanaandikisha wakulima ambao baada ya pembejeo kufika wanalipia Sh. 70,000 na kupewa mbolea.