Akizungumza wakati wa kukabidhiwa gari hilo na Mkurugenzi wa Radio One, Deogratius Rweyunga, mshindi huyo alisema haikuwa rahisi kuamini kama ameshinda kutokana na wimbi la utapeli lililopo kwa sasa.
“Nilipopigiwa simu kuambiwa nimeshinda gari. Sikuamini nikamwambia mke wangu naye hakuamini lakini baadaye wakanipigia tena simu wakaniambia nifike katika ofisi zao zilizopo Dar es Salaam, Mikocheni siku ya Ijumaa (jana).
“Baada ya kuambiwa hivyo, ilibidi nianze kujiandaa kuondoka Songea kuja Dar es Salaam, nikamchukua rafiki yangu ambaye anajua kuendesha gari kwa ajili ya kuliendesha wakati wa kurudi nyumbani
Nimecheza mara 12 na nimetumia elfu 12 tu mpaka kushinda gari kwa hiyo niwasihi vijana wenzangu wasikilize radio one na vipindi vyake wanaweza kuibuka washindi kama mimi,” alisema.
Miti alisema siku zote anayefanikiwa huwa anakuwa mtu wa kujaribu bila kujali matokeo kwa hiyo kwake hiyo inampa nguvu ya kuendelea kushiriki ili kujiweka katika nafasi ya kushinda vitu vingine.
Baba mdogo wa mshindi huyo, Festo Miti, katika hafla hiyo alimsihi kuitunza mali hiyo akibainisha kuwa katika familia yao hawajawahi kumiliki hata baiskeli kwa hiyo gari kwao ni kitu cha thamani.
“Nimemsihi mwanangu awe makini na marafiki lakini asimsahau mke wake ambaye wamesota wote katika kutafuta. Azidishe heshima kwa watu kupata gari isiwe sababu ya kuwadharau watu wengine,” alisema.
Rweyunga alimpongeza Miti kwa kuibuka mshindi katika kinyang’anyiro hicho huku akiwasihi watu kuendelea kuchangamkia fursa hiyo.
‘’Kwa wale wanaotaka kushinda zawadi zingine wasikilize vipindi vya Radio One wakiwa na laini za simu za mitandao ya Tigo, Vodacom, Airtel na Halotel kwa Sh. 1,000 tu huku wakibonyeza namba za menyu kulingana na mtandao wanaotumia kisha kwenda lipa bili. Baada ya hapo wanaingiza namba ya kampuni ambayo ni 222223 na baada ya hapo wataingiza kumbukumbu namba ambazo ni 111,au neno SUPA.
Tumekuwa na mchezo Supa toka Mei na tumekuwa tukitoa zawadi mbalimbali. Kadri tunavyozidi kwenda, ndivyo tunaboresha zawadi zetu. tulianza na Sh. 100,000 tumepanda mpaka ilifika wakati tunatoa Sh milioni tano mshindi huyo alitoka Mwanza,” alisema.










