Bil 4.5/- kunufaisha wakulima wa alizeti

09Oct 2022
Beatrice Moses
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Bil 4.5/- kunufaisha wakulima wa alizeti

MRADI wa Sh. bilioni 4.5 unaotekelezwa na Taasisi ya Kuboresha Mifumo ya Masoko ya Kilimo Tanzania (AMDT), unatarajia kuwanufaisha wakulima 100,000 wa mazao ya alizeti na mikunde walioko kwenye mikoa 11.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa AMDT, Charles Ogutu, alisema fedha hizo zitatolewa kama ruzuku kwa taasisi za serikali na mashirika wabia ambao wataongoza utekelezaji wa miradi kwenye mikoa hiyo.

Alisema uwekezaji huo mkubwa unalenga kusaidia kwenye vipaumbele vya serikali katika sekta mama ya kilimo kama ilivyoainishwa kwenye ajenda 10/30 na programu ya kuendesha sekta ya kilimo ASDP 11.

“Uwekezaji huu unalenga kuwawezesha wakulima kupata mbegu bora, kuunganishwa na huduma za biashara na fedha katika minyororo ya thamani ya alizeti  na mikunde.

“Pia kuboresha huduma za ugani, usimamizi wa mavuno na uchakataji wake na kuongeza thamani ya mazao haya, mikoa itakayonufaika ni Manyara, Singida, Morogoro, Dodoma, Lindi, Arusha Ruvuma, Songwe, Rukwa na Njombe," alisema.

Aliongeza kuwa miradi hiyo itatekelezwa hadi mwaka 2023 na endapo itakuwa na mafanikio, itaongezwa muda hadi mwaka 2024.

Ogutu alisema miradi hiyo itatekelezwa kwa kuzingatia masuala ya usawa wa jinsia na mbinu za kukabialiana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Pia alisema wanatarajia kufanya hamasa ya ulaji wa mazao ya kunde ikiwamo mbaazi, ambazo zimethibitishwa hupunguza udumavu wa akili. 

Mkurugenzi Mkazi wa Farm Africa, Mary Batterman alisema ni muhimu mkulima wa alizeti kupata mbegu bora kwa kuwa huinua kipato kutokana na mavuno mazuri yanayopatikana.

Mratibu wa alizeti kitaifa kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Frank Reuben alisema mahitaji ya mbegu bora ya alizeti ni mara 10 ya mbegu zinazozalishwa.

“Kuna fursa kubwa kwa kampuni za ndani na nje ya nchi kuwekeza katika eneo hili ili kuwezesha kupatikana kwa wingi mbegu bora kulingana na mahitaji yaliyopo,” alisema.