Serikali kuboresha barabara kuvutia watalii

04Mar 2024
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Serikali kuboresha barabara kuvutia watalii

​​​​​​​SERIKALI imesema inajenga  barabara ya kwenda Loliondo kwa kiwango cha lami ili kuvutia idadi kubwa ya watalii kutembelea vivutio vilivyoko ukanda wa Loliondo katika Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha.

Meneja wa Wakala wa Barabara, Mkoa wa Arusha (TANROADS), Reginald Massawe, amesema wakala huyo anakusudia kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili kupunguza gharama za usafiri na usafirishaji.

"Loliondo haifikiki kwa lami, hivyo tumekusudia kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami ili kupunguza gharama za usafiri na usafirishaji. Lakini kupunguza muda wa usafiri na usafirishaji mazao na mifugo kutoka ukanda huo, hasa kwa wakazi wa Wilaya ya Ngorongoro na Mji wa Loliondo na vitongoji vyake,"amesema Massawe.

Amesema kukamilika kwa barabara hiyo, kutaongeza thamani ya mazao na mifugo na kukuza kipato kwa wananchi waishio maeneo hayo, hivyo kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii katika nchi, hasa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

Kwa mujibu wa Meneja huyo, kwa mwaka wa fedha 2023/24, Mkoa wa Arusha, imepokea Sh. bilioni 1 .3 kwa ajili ya kazi za dharura, zilizotokana na uharibifu wa miundombinu iliyosababishwa na mvua za El-Nino.

Aidha, amesema serikali inatambua umuhimu wa kuunganisha makao makuu ya mkoa na makao makuu ya wilaya ili kuimarisha uchumi na shughuli za kijamii.