CCU kutumia bil 11 kumaliza uhaba wa mafuta nchini

04Mar 2024
Daniel Limbe
CHATO
Nipashe
CCU kutumia bil 11 kumaliza uhaba wa mafuta nchini

​​​​​​​CHAMA Kikuu cha Ushirika wilayani Chato mkoani Geita, Chato Co-operative Union (CCU) kinatarajia kutumia zaidi ya Sh. bilioni 11.5 katika mkakati wa kukabiliana na uhaba wa mafuta ya kula nchini.

Fedha hizo zinatarajiwa kutumika kununua pamba, kufunga mitambo ya kuchakata mafuta ya kula, kuzalisha mashudu pamoja na sabuni ili kufanya mafuta yapatikane wakati wote.

Kaimu Meneja wa Chama hicho, Berino Msigwa, amesema hayo wakati akiwasilisha makadirio na ukomo wa madeni kwenye mkutano mkuu wa mwaka 2024/25 wa chama hicho na kwamba hatua hiyo itasaidia kuongeza ajira kwa vijana na kuimarisha uchumi wa Kaya, Wilaya, Mkoa na Taifa kwa ujumla.

Kadhalika katika Mkutano huo wamechaguliwa wajumbe wapya wa bodi ya uendeshaji wa Chama hicho, ambapo msimamizi wa uchaguzi huo kutoka Tume ya ushirika makao makuu, Jackson Mushumba, amemtangaza Johnson Mudandu (Kilimo kwanza) kuwa Mwenyekiti baada ya kupata kura (60), Kulwa Lukuba Makamu Mwenyekiti kwa kura (20) Pamoja na wajumbe watatu ambao ni Emmanuel Ndalahwa, Petro Bikira na Mussa Method.

Mrajis Msaidizi wa Ushirika mkoani Geita, Doreen Mwanry, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Mandia Kihiyo, amewataka wanachama wa chama hicho kubuni miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia AMCOS zao badala ya kutegemea zao la pamba pekee na kwamba kinachotazamwa na serikali katika ushirika ni tija kwa wakulima.