Soko kubwa la madini Afrika Mashariki kujengwa Tunduru

03Mar 2024
Na Mwandishi Wetu
Tunduru
Nipashe Jumapili
Soko kubwa la madini Afrika Mashariki kujengwa Tunduru

HALMASHAURI ya Wilaya ya Tunduru kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wilayani humo ipo mbioni kukamilisha ujenzi wa soko jipya la kisasa la madini ya vito ambalo litakuwa ni soko kubwa zaidi Afrika Mashariki kwa madini ya vito.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Chiza Marando amesema ujenzi huo ulioanza mwishoni mwa Desemba 2023 unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Aprili 2024 na utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.087 na jengo litakuwa na uwezo wa kutumiwa na kampuni 155 za madini ya vito kwa wakati mmoja.

Marando amesema zaidi ya kampuni 130 zimeshaomba nafasi ya kufanyia biashara kwenye soko hilo na kwamba eneo la soko lina uwezo wa kubeba makampuni zaidi ya 500 ikiwa makampuni yataendelea kujitokeza.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Wakili Julius Mtatiro akiambatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya, ametembelea ujenzi huo na kupongeza hatua hiyo muhimu yenye tija kwa mustakabali wa rasilimali ambazo ziko Tanzania.