Rais Samia atoa zawadi kituo cha watoto yatima Shinyanga

04Jan 2024
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Rais Samia atoa zawadi kituo cha watoto yatima Shinyanga

RAIS Samia Suluhu Hassan amekabidhi zawadi mbalimbali kwa watoto yatima ambao wanalelewa katika Kituo cha Shinyanga Society For Ophans kilichopo Bushushu Manispaa ya Shinyanga.

Zawadi hizo zimekabidhiwa leo Januari 04, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Johari Samizi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme kwa niaba ya Rais Samia.

Samizi akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo amesema Serikali ipo bega kwa bega na wadau wa maendeleo ambao wamekuwa wakisaidia watoto hao Yatima kwa kuwapatia huduma ya malezi pamoja na elimu.

“Rais Samia hua anautaratibu wake kila sikukuu lazima awashike mkono watoto Yatima na wale ambao wanaishi katika Mazingira hatarishi, na katika kituo hiki amekabidhi zawadi ya mchele, sukari, mafuta ya kupikia, nguo pamoja na juice,” amesema Samizi.

Nao watoto Hao Yatima akiwamo Hadija Ally, wamemshukuru Rais Samia kwa kuwapatia zawadi hizo, na kuahidi wataendelea kumuombea kwa Mungu ili aendelea kuwa na Afya njema ili awatumikie watanzania na kuwasaidia watoto ambao ni Yatima.

Naye Meneja wa Kituo hicho cha watoto Yatima, Farhiya Said, ameshukuru kwa zawadi hizo, na kuipongeza Serikali kwa kuwaunga mkono, huku akiahidi wataendelea kuwapa watoto hao malezi bora pamoja na elimu, na kubainisha kwamba wana watoto 35, ambao wanasoma Shule za msingi ni 26 na Sekondari 9.