PURA yawaita watoa huduma kujisajili mfumo wa kidigitali

29Oct 2023
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
PURA yawaita watoa huduma kujisajili mfumo wa kidigitali

WATOA huduma, wasambazji na wataalamu katika sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia nchini wametakiwa kujisajili katika kanzidata maalum ya kidijitali ili kunufaika na fursa mbalimbali katika mnyororo huo wa thamani.

Mfumo huo wa kidigitali uliotengenezwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondoa Juu wa Petroli (PURA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), mpaka sasa umesajili jumla ya wataalamu wa ndani 300 and wasambazaji 1900.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, mkuu wa kitengo cha ushirikishaji wa wazawa na ujumuishaji wa wadau, Charles Nyangi alisema kulingana na kanuni na sheria za eneo hilo, Pura imeamriwa   kuanzisha kanzidata kwa wauzaji na watoa huduma kuwezesha wawekezaji kupata wataalam sahihi ikiwa ni pamoja na wahandisi wa mafuta ya petroli, wasambazaji, watoa huduma pamoja na washirika wa biashara za mafuta na gesi.

Aliongea hayo katika mkutano wa siku moja uliowaleta pamoja kampuni watoa huduma katika sekta hiyo ili kuwafundisha kwa kiona jinsi mfumo huo unvofanya kazi na ni kwa namna gani wanaweza kujisajili.

“Kanzidata hiyo inabeba na data zote zinazohitajika ni pamoja na wataalam katika sekta hiyo, tumeweka sifa zao za awali na kuweka taarifa sahihi kwa wawekezaji kupata wataalamu kwa urahisi wanapokuja nchini kuwekeza, katika Sekta hiyo na kuweza kukuza uchumi wa nchi,” Nyangi alisema.

Alibainisha  kuwa mchakato huo ulifanyika kwa umakini ili kuhakikisha wanaweka watu sahihi wanaohusika na kazi hizo na kuleta matokeo chanya rasilimali za mafuta na gesi.

Aidha  alisema ushiriki wa wazawa katika miradi ya petroli na gesi umeimarika hasa katika suala la ajira huku akiwahamasisha watanzania kuchangamkia fursa katika upande wa biashara hiyo.

Aliongeza kuwa  wanahamasisha wenyeji kushiriki katika sekta hiyo ambayo katika miaka iliyopita kazi nyingi zilifanywa na wageni kutokana na kutokuwepo mwamko katika masuala ya mafuta na gesi.

“Tumewaleta hapa leo, kampuni zinazofanya kazi katika mafuta na gesi ili kuwaelezea wa kina juu ya mfumo huu mpya wa kidigitali  ambao umechukua nafasi ya matumizi karatasi yaliyohitaji waendeshaji kuwasilisha mpango wao wa maudhui ya ndani na ripoti kila mwisho wa mwaka, kwa mfumo huu sasa ripoti zote zitakuwa zinatumwa kwa njia ya mtandao,” alisema.

Ally Mluge, ofisa maendeleo ya jamii wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) alisema mfumo huo mpya wa kidijitali ni muhimu kwani utasaidia kwa kiasi kikubwa makampuni na wadau kuwasiliana na mamlaka kwa urahisi hivyo kuokoa upotevu wa fedha na muda.