Amebainisha hayo wakati alipotembelea eneo la mradi huo wa ujenzi wa umeme wa jua katika kijiji cha Ngunga wilayani Kishapu akiwa ameambatana na Wakandarasi ambao wanatekeleza mradi huo, wadau kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa, wataalamu mbalimbali pamoja na wasimamizi wa mradi kutoka TANESCO.
Amesema utekelezaji wa mradi wa umeme huo wa jua wilayani Kishapu unatekeleza wa awamu ukiwa na Megawatts 150, ambapo kwa awamu ya kwanza utakuwa na Megawatts 50, na kumkata Mkandarasi katika utekelezaji wa mradi huo ahakikishe vijana ambao ni wazawa wa maeneo husika wanapewa kipaumbele cha ajira.
“Nakuagiza Mkandarasi wakati wa utekelezaji wa mradi huu hakikisha vijana kutoka hapa kijiji cha Ngunga eneo la mradi, vijana wa Kishapu na mkoa mzima wa Shinyanga, wanapata kipaumbele cha ajira ili wanaufaike na mradi na kuwainua kiuchumi,” amesema Mndeme.

“Kutekelezwa kwa mradi huu kunakuja kuondoa kabisa changamoto za Nishati ya umeme, kuongeza ajira hasa kwa vijana wa Mkoa wa Shinyanga na kuimarisha uchumi wa wananchi wetu, na haya ndiyo malengo ya Mhe. Rais wetu kwa Watanzania kuwaondolea kero zote na kuimarisha uchumi wao," ameongeza Mndeme.
Amemwagiza pia Mkandarasi huyo, kuukamilisha mradi huo kwa wakati ndani ya muda ambao umepangwa kwa kuzingatia ubora na viwango, ili wananchi waanze kunufaika kupata umeme wa uhakika na hakutakuwa na mgao tena.
Msimamizi wa Mradi huo wa Umeme wa Jua kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mhandisi Emmanuel Anderson, amesema wamejipanga vyema kuhakikisha wanamsimamia Mkandarasi huyo kuukamilisha mradi huo kwa wakati na viwango vinavyotakiwa.
Amesema mradi huo umechukua eneo zaidi ya Hekari 1000, na Wananchi waliopisha eneo hilo wameshalipwa fidia, na kwamba Mkandarasi kutoka Kampuni hiyo ya Sinohydro tayari ameshaini Mkataba wa miezi 17 ili kuukamilisha mradi huo ambao utagharimu zaidi ya Bilioni 323.
Naye Meneja Mradi kutoka Kampuni ya Sinohydro ambao ndiyo watekelezaji wa mradi huo wa umeme wa Jua wilayani Kishapu Tony Du, amemtoa wasiwasi Mkuu huyo wa Mkoa, kwamba mradi huo watautekeleza ndani ya wakati sababu uwezo wanao na wanavifaa vya kutosha, na kuahidi kutoa kipaumbele cha ajira kwa vijana wazawa.










