Operesheni hiyo hiyo iliyoanza jana katika wilaya ya Ilala, itakuwa endelevu ili kuhakikisha bidhaa hafifu zisizo na ubora yakiwamo matairi yanaondolewa sokoni.
Ofisa Uhusiano TBS, Roida Andusamile alisema kuwa awamu itakayofuata ya operesheni hiyo ni katika wilaya ya Kinondoni na Temeke jijini Dar es Salaam na kisha nchi nzima.
“Kiwango cha kimataifa cha matairi hakiruhusu matairi yaliyotumika sokoni, iwe ni kwa ajili ya matumizi ya baiskeli, magari au pikipiki, Watanzania tubadilike kwani matairi makuukuu huwa chanzo cha ajali nchini,” alisema Andusamile.
Mwenyekiti wa Chama cha wauza matairi makuukuu mkoa wa Dar es Salaam, Khatibu Mwinyi aliwaambia waandishi wa habari kwamba kuondolewa kwa matairi hayo sokoni kutaathiri watumiaji wengi wenye kipato cha chini na kati.
“Kuna nchi nyingi zinatumia matairi kama hayo kama Kenya , Brazil na kwingineko yanasaidia, mradi tu yasiwe chakavu sana, sababu tairi jipya ni ghali kutegemeana na aina ya tairi na kampuni yanakotoka, lakini ukija hapa kuna tairi hadi la Sh. 30,000 na kuendelea,” alisema Mwinyi.
Alisema wanaiomba serikali iwaruhusu kuuza mzigo mkubwa wamatairi waliyohifadhi stoo, kisha baada ya hapo watasitisha uuzaji wa matairi hayo.










