Mkurugenzi Mkuu TBL awaasa vijana

13Feb 2016
Sabato Kasika
Dar
Nipashe
Mkurugenzi Mkuu TBL awaasa vijana

VIJANA wametakiwa kufanyakazi kwa bidii na kwa uvumilivu na kuwa tayari kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo sehemu za kazi bila kusahau kujiendeleza kielimu.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni TBL Group Roberto Jarrin.

Wito huo ulitolewa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni TBL Group Roberto Jarrin kwenye hafla ya kuwatunuku vyeti wafanyakazi wa kampuni yake tanzu ya Tanzania Distilleries Limited (TDL) maarufu kama Konyagi walioitumikia kwa muda mrefu.

"Tuko hapa kwa ajili ya kuwapongeza wenzetu ambao wamefikia siku hii ya leo ya kupewa tuzo ya utumishi wa muda mrefu...ninaamini sote tukifanya kazi kwa bidii na kuwa na uvumilivu wa kukabiliana na changamoto tunazokabiliana nazo kwenye kazi zetu za kila siku tutafanikiwa kufikia hatua kama waliyofikia wenzetu ambao tunawapongeza siku hii ya leo," alisema Benjamin.

Benjamin aliwapongeza wafanyakazi hao kwa mchango wao mkubwa walioutoa katika mafanikio ya kampuni na kuwa na uvumilivu wa kukabiliana na changamoto mbalimbali walizokutana nazo katika kipindi cha utumishi wao.

"Wafanyakazi hawa ni mfano wa kuigwa na wengine hususani vijana ambao ni wengi katika kampuni kwa kufanya kazi kwa bidii na uvumilivu na kuwa tayari kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo sehemu za kazi bila kusahau kujiendeleza kielimu," alisema.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa wafanyakazi wote ni familia moja hivyo siku zote tutakuwa nao karibu na kuendelea kuwajengea mazingira mazuri ya kufanya kazi na kwamba watashirikiana ili kuendelea kupata mafanikio.

Akiongea kwa niaba ya wafanyakazi wenzake waliotunukiwa vyeti kwa utumishi wa muda mrefu wa kati ya miaka 10 hadi 35, Tatu Maganga ambaye ametumikia kampuni kwa miaka 35, alisema siri kubwa ya utumishi wa muda huo katika kampuni ya TBL ni kutokana na mazingira bora ya kazi yaliyopo.

"Tunashukuru kampuni kwa kuthamini mchango wetu wa muda mrefu tulioitumikia, tumeanza kazi tukiwa vijana mpaka tumekuwa na umri mkubwa tukiwa tunaitumikia kwa sababu ya mazingira bora ya kazi yaliyowekwa na mwajiri wetu," alisema Maganga.

Kufikia sasa zaidi wa wafanyakazi 50 wa kampuni ya TBL Group kutoka viwanda vyake mbalimbali wametunukiwa vyeti na zawadi kwa kutambua mchango wao wa utumishi wa muda mrefu.

Viwanda vingine vilivyopo chini ya kampuni hiyo ni viwanda vya kutengeneza bia vya TBL na DarBrew Limited kinachotengeneza kinywaji aina ya Chibuku.