Mikopo hiyo hutokana na mapato ya ndani na asilimia nne hutolewa kwa vijana na wanawake, huku asilimia mbili ikitolewa kwa watu wenye ulemavu.
Awali, mikopo hiyo ilisitishwa na serikali kwa ajili ya kufanyiwa maboresho lakini itaanza tena rasmi mwakani.
Naibu Waziri Katambi, alibainisha hayo wakati akizungumza na baadhi ya wajasiriamali wa Manispaa ya Shinyanga na kusema mikopo hiyo isiyo na riba itaanza kutolewa mwakani, hivyo waichangamkie ili wapate mitaji na kujikwamua kiuchumi.
“Serikali tayari imemaliza kuifanyia maboresho na Januari, mwakani, itaanza kutolewa tena. Itumieni kujikwamua kiuchumi kwa kufanya biashara mbalimbali kwa tija,”alisema Katambi.
Pia aliwakumbusha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao kwa kuwachagua viongozi makini, wachapakazi na wenye kupenda maendeleo, na si kuuza maendeleo kwa kuchagua kiongozi asiyestahili kwa sababu ya rushwa.
“Kura yako ndiyo maendeleo yako, tuache kuuza maendeleo kwa pesa, chagueni viongozi wenye uchungu na nyie,” alisema Katambi.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Johari Samizi, aliwasihi wanawake wasibweteke bali waichangamkie mikopo hiyo ambayo kwa sasa itaanza kutolewa hata kwa mtu mmoja mmoja na si lazima kikundi kama zamani na waitumie kufanya shughuli za ujasiriamali.
Baadhi ya wajasiriamali walimshukuru kwa kupatiwa elimu ya ujasiriamali na fursa zilizopo, ambazo wanaweza kuzitumia na kujikwamua kiuchumi.
Kuhusu mikopo hiyo, walitoa wito kwa serikali kuondoa milolongo mirefu kuipata ili kutosababisha wanawake kuendelea kujiingiza kwenye mikopo kausha damu.









