Milioni 964/- zaboresha huduma ya elimu Nzega

21Dec 2023
Halima Ikunji
NZEGA
Nipashe
Milioni 964/- zaboresha huduma ya elimu Nzega

ZAIDI ya Sh. milioni 964 zimetumika katika ujenzi wa shule mbili za sekondari na msingi katika Kata ya Mwasala, Halmashauri ya Nzega mkoani Tabora na kuondoa kero zilizokuwa zikiwakabili wanafunzi wa eneo hilo.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo, ofisa mipango wa halmashauri hiyo, James Raymond, alisema ujenzi wa shule za sekondari uligharimu Sh.milioni 603 na shule mpya ya msingi Mwandu ambayo imegharimu Sh.milioni 331.

Alisema hali hiyo umewaondolewa wanafunzi adha ya kutembea zaidi ya km 20 kufuata masomo katika kata ya jirani na kusababisha wengi wao kushindwa kuendelea na masomo.

“Zaidi ya nusu ya wanafunzi walikuwa wakishindwa kumaliza masomo ya darasa la saba huku kati ya wanaohitimu walishindwa kuendelea na masomo ya sekondari kutokana na shule kuwa umbali wa zaidi ya km 20,” alisema.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwasala, Jonas Kwiyera, alisema wastani wa watoto 50 hadi 100 walikuwa wanaacha shule kila mwaka kutokana na kutembea umbali mrefu na kuvuka mto ambao ulikuwa hatari kwao.

“Mfano kati ya wanafunzi 320 walioanza darasa la kwanza mwaka 2017 shuleni kwetu ambao waliomaliza darasa la saba ni 147 tu, hivyo tunashukuru serikali kwa kupata shule hii mpya kwani watoto wengi wanaotoka kijijini hapa ndio wanaongoza kwa kuacha shule,” alisema Mwl. Jonas.

Naye Ofisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Nzenga, Magesa Mgeta, alisema ujenzi wa shule hiyo mpya umesaidia kudhibiti utoro kwani hali ilikuwa mbaya ambapo kwa mwaka huu kati ya watoto 187 walioanza kidato cha kwanza mwaka jana waliofanya mtihani wa kidato cha pili ni watoto 47.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Modest Apolinary, alimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake njema ya kumaliza kero za wananchi katika sekta zote kwa halmashauri hiyo.

Alisema halmashauri hiyo imepokea zaidi ya Sh. bilioni mbili kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya halmashauri na Sh. bilioni moja za ujenzi wa hospitali mpya katika kijiji cha Lubisu Kata ya Utwigu na inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Desemba.