Arusha kujiandaa na tamasha kubwa la dansi

02Sep 2021
Neema Emmanuel
Mwanza
Nipashe
Arusha kujiandaa na tamasha kubwa la dansi

TAMASHA pekee kubwa la muziki wa dansi nchini lijulikanalo kama Usiku wa Wafia Dansi linatarajia kufanyika jijini Arusha mwezi Septemba mwaka huu.

Akiongea na Nipashe, Mratibu wa tamasha hilo Bernard James, amesema wakazi wa Arusha watapata fursa ya kuufaidi muziki wa dansi kwa mara ya kwanza kutoka kwa bendi zaidi ya nne.

Bernard amesema ni nadra bendi zaidi ya nne kutumbuiza jukwaa moja jijini humo kwa siku za hivi karibuni.

Kwa siku nyingi wakazi wa jiji hilo la kitalii hawajashuhudia bendi kibao zikichuana kwenye jukwaa moja na kukata kiu ya mashabiki, hivyo fursa hii itawapa la kufurahia na kujifunza.

Amesema tamasha hilo litawapa mashabiki nafasi ya kuamua ni bendi gani itakayoibuka kidedea kwa kushambulia vizuri jukwaa, kupendeza jukwaani, kuwa na nidhamu, kuwajibika, kuzingatia muda na kuwaibua vitini mashabiki.

"Kituo kikubwa cha runinga nchini kitarusha tamasha hilo mubashara, hivyo kila bendi ina wajibu wa kuwakuna vilivyo mashabiki wa muziki wa dansi jijini Arusha na dunia nzima itakayokuwa ikishuhudia tukio hilo" amesema Mratibu wa tamasha hilo.

Amezitaja baadhi ya bendi zitakazopanda jukwaani kukata kiu ya mashabiki wa dansi kuwa ni Bogoss Muzika chini ya Nyoshi El Saadat, Waluguru Original chini ya Killer Boy, Mjengoni Classic Band chini ya Digital Mukongya na Rickernest Band.

Tamasha hilo litafanyika tarehe 25 Septemba katika ukumbi wa Cocoriko Annex ndani ya viunga vya Tripple A kuanzia saa 2 usiku.

Mratibu huyo amewaomba wadhamini mbalimbali kujitokeza kudhamini tamasha hilo ili kuukuza muziki wa dansi.

"Kwa sababu tukio lote litarushwa live na kituo kikubwa cha luninga nchini, hii ni fursa kwa wadhamini mbalimbali  kujitokeza kunadi bidhaa na shughuli zao lakini kusaidia pia tukio hilo lifanikiwe na wanamuziki watakaoshiriki wanufaike zaidi" amesema Mratibu wa tamasha hilo

Baadhi ya wadhamini wa tukio hilo ni Cheza Kidansi Entertainment, Cocoriko Annex pamoja na Mo Green International.

Tamasha hili lilianza mwaka 2018 na linafanyika mara ya nne baada ya kufanyika jijini Dar es Salaam, Mwanza, Morogoro na sasa Arusha.