Serikali ihakikishe Katiba mpya inapatikana kabla mwaka 2020

08Jul 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali ihakikishe Katiba mpya inapatikana kabla mwaka 2020

KATIKA toleo letu la jana, tulichapisha habari ikieleza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) inatarajia kukamilisha mchakato wa katiba inayopendekezwa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Mwenyekiti wa Nec, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi na kusema Katiba inayopendekezwa itaweka maoni ya wananchi juu ya mapendekezo ya kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi wanayoitaka, hivyo katika uchaguzi ujao kutakuwapo na tume huru ya uchaguzi.

Alisema ili kufanyika kwa kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa, ni lazima kwanza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) na Nec zikutane ili kufanya marekebisho ya sheria ya taifa ya uchaguzi.

Alisema ili kupata tume ya uchaguzi ambayo itakuwa huru, itatokana na kupatikana kwa katiba mpya ambayo mchakato wake unatarajiwa kumalizikia kwenye kura ya maoni.

Kwa muda mrefu Watanzania wamekuwa na kiu ya kupata katiba mpya ili iendane na wakati uliopo sasa, kwani katiba iliyoko ni ya takribani miaka 50 iliyopita.

Baada ya kuanzishwa kwa mchakato wa katiba mpya, wananchi wengi walijenga matarajio kwamba katiba mpya ingepatikana kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.

Kwa bahati mbaya, ahadi iliyotolewa na Serikali kwamba Tanzania ingepata katiba mpya kupitia kura ya maoni ambayo ingefanyika Aprili 30, 2015, ilishindikana kutokana na kutokukamilika maandalizi yake pamoja na mambo mengi ya msingi kuingiliana.

Miongoni mwa mambo hayo ni kuchelewa kukamilika kwa uandikishaji wa wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kupitia mfumo wa kielektroniki (BVR) na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Pamoja na wananchi kadhaa kueleza kutoridhishwa na kutokupatikana kwa katiba mpya, lakini vilevile walikatishwa tama na jinsi Bunge Maalum la Katiba lilivyoendeshwa na kumalizika katika hali ya mpasuko mkubwa, kutokana na wajumbe kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kulisusia kwa tuhuma mbalimbali.

Aidha, kuondolewa kwa mambo kadhaa ya msingi yaliyoingizwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika Rasimu ya Katiba, ni jambo lingine ambalo linalalamikiwa na makundi kadhaa nchini.

Miongoni mwa mambo hayo ni masharti ya maadili kwa viongozi wa umma, mawaziri kutokuwa wabunge, ubunge kuwa na ukomo, wabunge kuwekewa kiwango cha elimu na wapigakura kupewa mamlaka ya kumwadabisha mbunge wao watakapoona ameshindwa kuwajibika.

Tunaamini kuwa Serikali itakuwa na nia ya dhati ya kukamilisha mchakato wa katiba mpya kwa wakati kama alivyoahidi Rais John Magufuli kuwa ataendelea alikoachia Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Hata hivyo, tunaishauri Serikali kwa kushirikiana na Nec kuharakisha maandalizi ili katiba ipatikane kabla ya mwaka 2020 ili uchaguzi utakaofanyika mwaka huo katiba hiyo itumike.

Tunashauri pia mambo ya msingi yenye maslahi kwa taifa yakiwamo masharti kuhusu maadili kwa viongozi wa umma yaingizwe kwa kuwa yatasaidia kurejesha maadili kwa uongozi wa umma kama Rais Magufuli anavyofanya kwa sasa.

Kuna mambo mengine mazuri ambayo Serikali ilishaeleza azma yake ya kutaka yaingizwe katika Katiba nayo ni tume huru ya uchaguzi, kuruhusu wagombea binafsi, matokeo ya urais kupingwa mahakamani na mshindi wa urais kutakiwa kuwa na kura zaidi ya asilimia 50.

Hayo yote yakipewa nafasi tunaamini kuwa Watanzania wengi wataipitisha Katiba inayopendekezwa kupitia kura ya maoni ili Katiba mpya ipatikane na kuanza kutumika.

www.guardian.co.tz/circulation