Kamishna na Mapato ya Ndani wa TRA, Elijah Mwandumbya, alisema juzi wakati wa tathmini ya ukusanyaji wa mapato kuwa hadi sasa wameshagawa EFDs 1,700 nchi nzima huku kwa mkoa wa Dar es Salaam wakigawa mashine 1,120.
Pia, mamlaka hiyo itafanya ukaguzi wa Namba ya utambulisho ya Mlipa kodi (TIN) ili kuwabaini wafanyabiashara wenye namba hizo zaidi ya moja. Kadhalika aliwataka wafanyabiashara wa vituo vya mafuta kuhakikisha ifikapo Oktoba Mosi wawe wamefunga mashine za kutolea risiti katika vituo vyao.
Uamuzi wa TRA wa kupita katika sehemu zote za biashara kukagua kama wafanyabiashara wanaotakiwa kuzitumia mashine hizo wanazitumia ni mzuri na umekuja wakati mwafaka, kwa sababu Serikali ilitoa agizo hilo kwa muda mrefu.
Kilichokuwa kinaonekana ni kwamba wafanyabiashara wengi walikuwa wanapinga matumizi ya mashine hizo kwa kutoa sababu mbalimbali, mojawapo ikiwa ni kulalamikia gharama zake kwamba ni kubwa.
Msisitizo wa TRA na Serikali kwa wafanyabiashara kuanza kuzitumia ulipingwa karibu na wafanyabiashara katika mikoa yote nchini na kubaya zaidi ni kuwa wengi waligoma na kufunga maduka, hatua iliyosababisha usumbufu mkubwa.
Serikali ya Awamu ya Tano ambayo miongoni mwa mambo inayoyapa kipaumbele na msisitizo mkubwa ni suala la kukusanya mapato.
Kutokana na hali hiyo, matumizi ya EFDs sio tena suala la hiyari bali ni lazima na ndiyo maana TRA imetangaza kuwafuatilia wafanyabiashara popote waliko kubaini kama wanazitumia ama la.
Ni matumaini yetu wafanyabiashara wote ambao wanatakiwa kisheria kuzitumia kuhakikisha kuwa wanaanza kuzitumia na kama kuna changamoto waziwasilishe TRA badala ya kuzikwepa.
Ni vizuri wakatambua kuwa Serikali haina nia ya kuwakomoa bali inatimiza jukumu lake la msingi la kukusanya mapato kwa ajili ya kujiendesha na pia kutoa huduma za msingi kwa jamii.
Hili linathibitishwa na hali iliyotokea katika miaka ya karibuni kwa Bunge kuidhinisha bajeti kwa ajili ya wizara mbalimbali, lakini fedha zilizopelekwa kutekeleza miradi ya maendeleo zilikuwa ni kidogo sana kutokana na Serikali kutokuwa na fedha za kutosha. Sababu ni kuwa ukusanyaji wa mapato haukuwa makini.
Ili Serikali ipate fedha za kutosha kutekeleza ahadi mbalimbali ilizotoa, itabidi iwe makini kuhakikisha inakusanya mapato ya kutosha na wafanyabiashara wakiwa watu muhimu kulipa kodi ya Serikali.
Huko nyuma wafanyabiashara wengi walikuwa wanakwepa kulipa kodi na kuikosesha Serikali mapato, hivyo tumaanini kuwa kama kila mfanyabiashara atatumia mashine hiyo hatakuwa na sababu za kukimbizana na TRA na mapato ya nchi yataongezeka.
Taarifa ya Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, kuwa makusanyo kwa mwezi Juni yamefikia Sh. trilioni 1.414 ikiwa imevuka lengo walilojiwekea la kukusanya Sh. trilioni 1.311 zinatia moyo kwamba jitihada za kukusanya kodi zikiendelea, mapato hayo yataongezeka zaidi.
Ushauri wetu ni kwamba wafanyabiashara washirikiane na TRA kutekeleza utaratibu huo na itakuwa vizuri kama mamlaka itaendelea kutoa elimu kwao kuhusu matumizi ya EFDs sambamba na maofisa wake kutowaonea wafanyabiashara.










