Mashuhuda kadhaa walieleza kuwa ajali hiyo ilisababishwa na uzembe wa madereva wa mabasi hayo moja kutoka Kahama mkoani Shinyanga na lingine kutokea Dar es Salaam ambao inadaiwa kuwa walikuwa wakifanya mbwembwe kwa lengo la kutaka kusalimiana.
Kwamba madereva wa mabasi hayo wana kawaida ya kuzungusha magari ili washikane mikono kila mabasi ya kampuni hiyo wanapokutana njiani, na kwamba ndicho kilichotokea juzi na kugharimu maisha ya abiria wasio na hatia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka, naye amesema kuwa ajali hiyo ilisababishwa na uzembe wa madereva hao. Kadhalika, Kamanda wa Kikosi cha Usalama wa Barabarani nchini, Mohamed Mpinga, naye amesema kuwa ajali hiyo ilitokana na uzembe wa madereva hao.
Kwa kweli ajali hiyo imetokea wakati Watanzania walikuwa wameanza kusahau matukio ya ajali za mabasi zilizokuwa zikitokea kila uchao katika maeneo mbalimbali nchini.
Jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) kwa kiasi kikubwa zilisaidia kupunguza wimbi la matukio ya ajali za mabasi. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na kusaidia kupunguza ajali hizo ni kuzuia mabasi kusafiri usiku, matumizi ya tochi na kamera.
Kutokea kwa ajali ya juzi pamoja na ajali mbili zilizotokea wiki iliyopita na kusababisha vifo vya watu 12 mkoani Morogoro kunatukumbusha kwamba kuna haja kwa mamlaka husika hususan Jeshi la Polisi kuongeza jitihada na ikiwezekane waongeze doria.
Ajali zilizosababosha vifo hivyo zilizotokea katika eneo moja la VETA Dakawa, Tarafa ya Dumila, Wilaya ya Kilosa.
Ajali ya kwanza ilitokea saa 11:30 jioni Juni 30 na kuua watu watano kufuatia malori mawili, mojawapo likiwa na shehena ya mafuta kugongana kisha kuwaka moto.
Ajali ya pili ilitokea hapo hapo saa 10:00 alfajiri ya Julai Mosi baada ya basi la kampuni ya Otta High Class kuligonga lori la mafuta lililokuwa likiungua moto na kusababisha vifo vya watu saba.
Ajali hizo sambamba na ripoti ya Kamanda Mpinga kuwa ndani ya wiki moja zimetokea ajali tatu zilizosababisha vifo vya watu 41 na kuwajeruhi wengine 73 na ni changamoto ambayo inahitaji kufanyiwa kazi ili taifa lisiendelee kupoteza nguvu kazi.
Tunawashauri madereva kuwa makini kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani. Madereva wa mabasi wanapaswa kuzingatia kuwa wanawasafirisha binadamu wanaotegemewa na familia na taifa kwa ujumla, hivyo watambue kuwa wana wajibu wa kuhakikisha wanalinda maisha yao badala ya kufanya mzaha na mambo mengine yanayoweza kusababisha ajali za kijinga na kupoteza maisha yao.
Tunaipongeza Sumatra kwa kutoa adhabu kwa mabasi ambayo yamebainika kukiuka sheria mbalimbali. Jana mamlaka hiyo ilitangaza kuyafungia mabasi yote City Boys, Otta High Class na Mohamed Trans kwa makosa mbalimbali yakiwamo ya ubovu wa mabasi na huduma mbovu hadi ukaguzi utakapokamilika.
Ni matumaini yetu kuwa mamlaka husika zitachukua hatua zaidi ili liwe fundisho kwa makampuni ya mabasi yote yanayokiuka sheria, kanuni na taratibu za barabarani na kusababisha ajali kutokana na uzembe wa madereva wao.










