Kwa mara nyingine Tanzania itawakilishwa na michezo mbalimbali ikiwemo Riadha ambayo mara kwa mara imekuwa ikishiriki bila ya kufanya vizuri.
Nipashe tunaamini maandalizi mazuri yanatoa nafasi kwa wanamichezo wetu kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali.
Tunawapongeza wale wote waliopata nafasi ya kufuzu kwa michezo hiyo lakini ni lazima tuseme wazi kuwa tunaimani wana uwezo wa kufanya vizuri katika michezo hiyo kama wana nia ya dhati.
Waende kwenye michezo hiyo kwa lengo moja tu la kufanya vizuri na kupeperusha vyema bendera ya nchi yetu.
Hakuna haja ya malumbano kwa vyama vya michezo shiriki na waratibu wa michezo hiyo hapa nchini, Kamati ya Olimpiki (TOC).
Kama kuna upungufu wowote ni wakati huu wanatakiwa kukaa pamoja na kuangalia njia bora za kusiadiana hili jina la
Tanzania lipate nafasi ya kupaa juu kwenye michezo hiyoa ambayo kwa muda mrefu tumekuwa tukitoaka kappa huku visingizio vikiwa vingi kuliko ukweli halisi.
Lakini pia Nipashe tunawakumbusha wahusika kuwa hakuna njia ya mkato kwenye mafanikio, lazima jasho liwatoke kupata mafanikio.
Wapo wanamichezo ambao wamefuzu muda mrefu kushiriki michezo hii hao ndio tunaimani nao kuwa wanaweza wakatuwakilisha vyema.
Bado kipindi cha chini ya mwezi mmoja kuanza michezo hii mikubwa Duniani, si vibaya kuwakumbusha wanamichezo yetu idadi ya matumaini ya watanzania waliopo nyuma yao ambao wataifuatilia kwa karibu michezo hii.
Nipashe, tunasema mkatuwakilishe vyema kwenye michezo hii, na uwakilishi mzuri unaanzia kwenye maandalizi ya sasa mneyoendelea nayo, nidhamu, kujituma na maarifa mtakayoyaonyesha sasa kwenye maandalizi yenu ni wazi yatahakisi kile mtakachoenda kukifanya Brazil kwenye jiji la Rio de Janeiro.
Idadi kubwa ya Watanzania tutakuwa nyuma yenu tukiamini mtarudi na kitu cha kujivunia na kitakachoipa sifa nchi yetu.
Na pia tunatoa wito kwa viongozi wa Serikali kuwa karibu na wanamichezo watakaotuwakilisha kuanzia sasa na kuacha kasumba na utamaduni wa kuwasubiri kuwakabidhi bendera ya Taifa wakati wakisafiri na kuwasubiri kuwapokea kwa sifa pale wanapofanya vizuri.
Nipashe tunawatakia maandalizi mema wanamichezo wote watakaoshiriki kwenye michezo hii na tunaimani mtafanya vizuri pamoja na kuwa wapo wanariwatabilia kufanya vibaya.
Maneno ya watu hao yasiwakatishe tamaa na badala yake iwe chachu kwenu kufanya vizuri na kuwajibu wale wote wanaowaona kama wasindikizaji kwenye michezo hii.










